Sifa ambayo mtu unajijengea, ina mchango mkubwa sana kwenye mafanikio au kushindwa kwako.
Kuna watu wanashangaa kwa nini mambo yao hayaendi sasa, lakini wamesahau ambayo wamewahi kufanya huko nyuma na sasa ni kikwazo kwao.
Ili kuhakikisha hujijengei sifa mbaya inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, hapa kuna mambo matatu muhimu ya kuzingatia kwenye Safari yako ya mafanikio.
Jambo la kwanza ni kutekeleza kila unachoahidi, bila ya kujali inakugharimu kiasi gani. Iwe ni mambo madogo au makubwa, ukishaahidi basi tekeleza kama ulivyoahidi. Watu wataona hilo na watakupa heshima na kukuamini kwa sababu wanajua ukisema unafanya. Kwa kifupi neno lako linapaswa kuwa sheria kwako mwenyewe.
Jambo la pili ni kutaka ushindi kwa kila mtu. Kwa kila unachofanya, usiangalie tu wewe unapata au kunufaikaje, bali angalia wengine nao wanapata na kunufaika na nini. Kwa kila jambo unalojihusisha nalo, hakikisha kila anayehusika anatoka na ushindi. Unaweza kupambana ukaondoka na ushindi, huku wengine wakitoka wameshindwa, lakini jua sifa yako haitakuwa nzuri, baadaye watu watakukwepa maana wanajua unaangalia ushindi wako tu. Unapojali na kuhakikisha wengine nao wanapata ushindi, watu wanakuheshimu na kukuamini na kuwa tayari kushirikiana na wewe.
Jambo la tatu ni kuwa tayari kuacha, hata kama inakugharimu. Kuna wakati unakutana na hali fulani ambazo zinaweza kukunufaisha, lakini zinakwenda kinyume na misingi yako, kuwa tayari kuacha na kuondoka hata kama itakugharimu au utapoteza manufaa. Unaweza kuona ni hasara, lakini ni kwa muda mfupi, baadaye inakujengea heshima na kukupa fursa kubwa zaidi. Maana watu wanajua hujali tu kupata, bali kuna misingi ambayo pia unaisimamia.
Zingatia haya matatu kwenye kila unalofanya kwenye maisha yako, na hutajiwekea vikwazo kwa baadaye. Utajijengea heshima na imani kwa kila unayejihusisha naye na utaweza kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha kwa makala nzuri Sana,inayotufundisha namna bora ya kujijengea heshima kwenye jamii zinazotuzunguka.
LikeLike
Karibu Datius.
LikeLike