Umekuwa unayatoroka maisha, kwa kuepuka kuishi leo na kukimbilia kuishi jana na kesho.
Kwa kuwa ugumu wote wa maisha yako unakabiliana nao leo, ni rahisi kujikumbusha mazuri yaliyopita au kujiliwaza kwa mazuri unayotegemea yawe.
Lakini hilo halitatui ugumu unaokabiliana nao.
Unakuwa unajidanganya tu, kwa sababu jana haitajirudia na hiyo kesho haitakuja kama unavyoitazamia, hasa kwa kutokufanya chochote leo.
Hii pia ni njia nzuri ya kuwapima wafanyaji na wasemaji. Wafanyaji watakuambia wanafanya nini sasa, wamekwama wapi sasa na hatua zipi wanazochukua. Lakini wasemaji watakuambia walifanya nini kipindi cha nyuma au wanategemea kufanya nini siku zijazo. Hawazungumzi chochote kuhusu leo, kwa sababu hakuna wanachofanya, hakuna ushahidi wanaoonesha.
Na yoyote watu wanayokuambia kuhusu jana yamejaa uongo mwingi, anaweza kuwa alikutana na bahati fulani na yeye akahesabu ni juhudi zake. Kumbukumbu zetu binadamu kwenye mambo yaliyopita huwa siyo nzuri, tunakuza mchango wetu na kupuuza mchango wa wengine, mazingira na bahati.
Kadhalika hatupo vizuri kwenye mipango yetu kwa siku zijazo, kila tunachopanga huwa kinaenda tofauti na tulivyopanga, kwa sababu hatujui nini kitakachotokea kesho.
Kitu pekee tulicho na uhakika nacho ni leo, kile tunachofanya sasa kwenye wakati tulionao. Na wengi hakuna wanachofanya, zaidi ya kupoteza muda, wakikumbuka mazuri ya nyuma na kutazamia makubwa yajayo.
Tasnia nzima ya uhamasishaji imejengwa kwenye mambo yaliyopita na yajayo, siyo kwenye mambo yaliyopo sasa. Kila mtu ni rahisi kusema nilianzia pale nikafika hapa, au niko hapa na nataka kufika kule. Lakini hakuna anayesema nafanya hiki sasa. Hiyo ni kwa sababu sasa haihamasishi, watu hawapendi hadithi za sasa, kwa sababu hazina nafasi ya uongo.
Weka mkazo wako kwenye sasa, chukua hatua sasa na usipoteze muda wako kwenye yaliyopita au yajayo. Ukiishi vizuri leo, kwa kufanya kilicho sahihi, utaweza kukabiliana na namna yoyote kesho itakavyokuja.
Kadhalika usidanganyike na hadithi za watu kwenye yale yaliyopita, au yajayo, bali angalia kile wanachofanya sasa. Haijalishi mtu anasema nini au anashawishi kiasi gani, kama huwezi kuona anachofanya sasa, jua jana anayokuambia au kesho anayokuahidi ni uongo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Watu hawapendi hadithi za sasa,kwa sababu hazina nafasi ya uongo.Ni kweli kabisa.
Asante Sana Kocha🙏🙏
LikeLike
Karibu.
LikeLike