“If I am to listen to another man’s opinion, it must be expressed positively. Of things problematical I have enough in myself.” – Johann Wolfgang von Goethe

Tayari una matatizo ya kutosha kwenye maisha yako, ya nini kuendelea kutafuta matatizo zaidi?

Tayari una mengi hasi yanayoendelea kwenye maisha yako, ya nini kuendelea kutafuta habari ngingine hasi zaidi?

Kwa namna maisha yako yanavyoenda, tayari umeshakutana na mengi ya kukukatisha tamaa, ya nini kuendeleza watu wanaokueleza mambo ya kukata tamaa muda wote?

Ni rahisi kutengeneza matatizo mapya, kutafuta habari hasi zaidi na kuwasikiliza wakatishaji tamaa, kwa sababu kufanya hivyo kunakusumbua, kunakufanya usiliangalie tatizo hasa.

Na kwa kuwa tatizo ni wewe, hutaki kulikabili, hivyo unaendelea kujificha nyuma ya kuyafanya mambo yawe magumu zaidi.

Kama unachotaka ni kuyafanya maisha yako kuwa bora, basi acha kutengeneza matatizo zaidi.
Ukishajikuta upo kwenye shimo, hatua ya kwanza ni kuacha kuchimba.
Lakini hivyo sivyo wengi wanavyofanya, badala ya kuacha kuchimba, wanakazana kuchimba zaidi.

Wanajua wakiacha kuchimba, watapata nafasi ya kufikiria jinsi ya kupanda juu kutoka kwenye shimo hilo, zoezi ambalo ni gumu kuliko kuchimba.
Ili wasipate nafasi ya kufikiria hivyo, wanatafuta cha kuwasumbua na kuwaweka bize zaidi, hivyo wanaendelea kuchimba.

Kagua kila unachofanya kwenye maisha yako, na jiulize unakifanya kwa sababu kinapelekea maisha yako kuwa bora zaidi au kinakuweka bize usione jinsi maisha yako yamevurugika?

Unapozurura kwenye mitandao ya kijamii siku nzima, ni kwa sababu inakufanya kuwa bora zaidi au kwa sababu hutaki kuikabili kazi yako?
Unapofuatilia maisha ya wengine, hasa wale wanaoteseka, ni kwa sababu unawaonea huruma au kwa kuwa unajisikia vizuri maisha yako hayakafikia hatua kama zao?

Matatizo uliyonayo mpaka sasa, tayari yanatosha kukuweka bize kuyatatua, acha kuyatoroka kwa kutengeneza matatizo zaidi, tatua hayo uliyonayo sasa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu mbwa anayetembea kwa miguu miwili, fungua hapa kusoma; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/12/2082

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.