Kuhangaika na mambo madogo madogo kwenye maisha yako ndiyo kikwazo kwako kuhangaika na mambo makubwa na yatakayokuwezesha kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Unaweza kujishangaa, iweje upoteze muda, nguvu na umakini wako kwa mambo yasiyo na tija, huku kukiwa na mambo mengine yenye tija. Kuna mambo matatu yanayopelekea hali hiyo.

Jambo la kwanza ni kutokuyachagua na kuyapangilia malengo yako vizuri. Malengo yanakuwa hayajatoka ndani yako kweli, bali umeiga kwa wengine au umekuwa nayo kwa sababu wengine wanataka wawe nayo. Hilo linakukosesha msukumo wa kuyafanyia kazi malengo yako, kwa sababu hujayachagua mwenyewe na hujayapangilia vizuri.

Jambo la pili ni kukosa ujasiri wa kuyasimamia malengo yako, hasa pale unapokutana na ugumu au changamoto. Hakuna asiyekutana na hali hizo, ila wasio na maandalizi wanapokutana na hali hizo hutoroka na kwenda kwenye mambo rahisi. Hapo wanaacha yaliyo magumu na kuhangaika na mambo rahisi.

Jambo la tatu ni kutaka raha ya haraka badala ya furaha ya muda mrefu. Mambo madogo madogo huwa yanaleta raha ya muda mfupi, lakini ni kikwazo kwenye furaha ya muda mrefu. Lazima uwe tayari kuikataa raha ya muda mfupi, kama unaitaka furaha ya muda mrefu.

Kama utayachagua na kuyapangilia malengo yako vizuri, ukawa na ujasiri wa kuyasimamia licha ya magumu unayokutana nayo na ukaondokana na hali ya kutaka raha ya muda mfupi, utaweza kusumbuka na yale makubwa na muhimu kwako na mambo madogo madogo hayatapata nafasi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha