Ni rahisi kutoa ushauri kwa wengine, lakini ni vigumu wewe mwenyewe kuuishi ushauri unaowapa wengine.
Hata pale mambo yanapowatokea watu wengine, ni rahisi kwetu kuwashauri na kuwapa moyo, lakini mambo hayo hayo yanapotutokea sisi wenyewe hatuwezi kutumia ushauri ambao tumekuwa tunawapa wengine.
Kinacholeta hali hizi za tofauti ni hisia ambazo mtu unakuwa nazo.
Pale jambo linapokutokea wewe mwenyewe, hisia zako zinakuwa kwenye jambo hilo na zinakuwa juu. Hali hiyo inapelekea usiweze kufikiri kwa usahihi na ndiyo maana hata ushauri ambao umewahi kuwapa wengine hautaweza kuutumia.
Lakini jambo linapotokea kwa mtu mwingine, hisia zetu zinakuwa hazipo kwenye jambo hilo, hivyo tunaweza kufikiri kwa usahihi na kuona hali ilivyo bila ya kuzuiwa na hisia. Tunapoona hali ilivyo, inakuwa rahisi kwetu kushauri hatua sahihi za kuchukua.
Kwa kujua udhaifu huu tulionao, inaweza kutusaidia tukaweza kujishauri vizuri wenyewe na kuvuka kila aina ya changamoto tunazokuwa tunapitia.
Unapojikuta kwenye hali yoyote ile, kwanza usikimbilie kwenye hitimisho, jipe muda wa hisia zako kuwa kwenye hali hiyo, lakini katika kipindi hicho jizuie usifanye maamuzi yoyote.
Baadaye tulia na ondokana na hisia hizo, kisha anza kuangalia hali hiyo kama vile unamwangalia mtu mwingine. Ona kile kilichotokea kama vile kimetokea kwa mtu mwingine, kisha jiulize ungemshaurije mtu huyo. Sahau kabisa kwamba kitu hicho kimetokea kwako na ona kimetokea kwa mtu mwingine.
Ni zoezi gumu kufanya, lakini lina matokeo mazuri. Ukiweza kuvuka hisia zako na kuangalia kilichotokea kama ambavyo kinaonekana na watu wengine, utaweza kufikiri kwa usahihi na kuziona hatua sahihi kwako kuchukua.
Hatua sahihi zipo mbele yako mara zote, ni hisia zako ndiyo zimekuwa kikwazo kwako kuziona hatua hizo. Kazana kuzivuka hisia zako pale unapojikuta kwenye changamoto mbalimbali ili uweze kuchukua hatua sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,