Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Mindset: the new psychology of success kilichoandikwa na mwanasaikolojia Carol S. Dweck.

Hiki ni kitabu kinachoelezea mitazamo ambayo watu tunayo na jinsi inavyoathiri maisha na mafanikio yetu.

Kupitia kazi zake, tafiti mbalimbali na maisha ya wengine Carol anawagawa watu kwenye makundi makuu mawili;

Kundi la kwanza ni wale wenye MTAZAMO MGANDO ambao anauita FIXED MINDSET.

Huku kundi la pili wakiwa wale wenye MTAZAMO WA UKUAJI ambao anauita GROWTH MINDSET.

Tofauti hii moja na ndogo tu kwenye mtazamo, ndiyo inaleta tofauti kubwa kwenye maisha kati ya wale wanaofanikiwa sana na wale wanaokuwa na maisha ya kawaida.

Mtazamo ambao mtu unakuwa nao, uwe ni mgando au wa ukuaji, unatokana na imani ambazo umekuwa nazo kwa maisha yako yote. Imani hizo hujengeka mapema tangu ukiwa mdogo, kulingana na mazingira yanayokuzunguka.

Kile ambacho wengi tunaita haiba, ni mtazamo wa kuendesha maisha ambao mtu unakuwa umeuchukua na kwenda nao maisha yake yote. Na kitu ambacho kimekuwa kikwazo kwa wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao, ni aina ya mtazamo wanaokuwa nao.

Kwenye kitabu hiki, Carol anakwenda kutuonesha jinsi mitazamo tuliyonayo inavyojengwa, jinsi inavyokuwa kikwazo kwa mafanikio na pia jinsi ya kubadili mtazamo ambao mtu unao na kuwa na mtazamo bora zaidi.

Kitabu kimesheheni tafiti mbalimbali pamoja na mifano ya wale waliofanikiwa na kushindwa kwenye michezo, biashara na hata elimu, kutokana na aina ya mtazamo ambao mtu anakuwa nao.

Kitabu pia kinatusaidia jinsi ya kuwajenga watoto kwenye mtazamo sahihi ambao utawawezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.

Kuhusu mwandishi.

Carol S. Dweck (kuzaliwa Oktoba 17, 1946) ni mwanasaikolojia wa nchini Marekani. Ni profesa wa saikolojia kwenye chuo kikuu cha Stanford lakini pia amefundisha kwenye vyuo vikuu vikubwa kama Columbia, Harvard na Illinois.

Carol anafahamika zaidi kupitia tafiti zake kwenye eneo la uwezo wa binadamu pamoja na motisha. Ni kupitia kazi hizo ndiyo ameweza kuja na kitabu hiki kinachoelezea aina mbili za mtazamo ambao watu wanakuwa nayo na jinsi zinavyoathiri mafanikio yao.

Karibu kwenye uchambuzi.

Uchambuzi wa kitabu hiki utakuwa na sehemu tatu;

Sehemu ya kwanza tutajifunza kwa kina kuhusu aina mbili za mtazamo ambao watu tunakuwa nao, kisha tutaingia ndani zaidi kwenye kila mtazamo na kisha kuona jinsi mitazamo hiyo inavyoathiri uwezo ambao mtu anakuwa nao.

Sehemu ya pili tutaona jinsi mitazamo ambayo watu wanayo inavyokuwa na madhara kwenye michezo, biashara na mahusiano. Kwenye michezo tutaona jinsi mitazamo inavyowatofautisha wanaoshinda na wanaoshindwa, kwenye biashara na kazi tutaona mitazamo inavyowajenga au kuwabomoa viongozi na kwenye mahusiano tutaona jinsi mitazamo inavyochangia kuimarika au kuvunjika kwa mahusiano.

Sehemu ya tatu tutajifunza jinsi mitazamo inavyojengeka kuanzia utotoni, tukiona michango ya wazazi, walimu na makocha katika kujenga mtazamo wa mtoto. Na mwisho tutajifunza jinsi mtu unavyoweza kubadili mtazamo wako kutoka mtazamo mgando kwenda mtazamo wa ukuaji ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha MINDSET, uweze kujua aina mbili za mitazamo, kujua mtazamo ulionao na jinsi unavyoathiri mafanikio yako na hatimaye kubadili au kuboresha mtazamo wako ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Tofauti kuu za mitazamo miwili kwa ufupi.

Mitazamo miwili ambayo watu wanayo, yaani mgando na ukuaji huwa inaleta tofauti nyingi kwa watu, lakini kubwa kabisa na zinazopelekea baadhi kufanikiwa na wengi kushindwa ni hizi;

1. UWEZO WA KIAKILI.

MGANDO; huona uwezo wa akili una ukomo na hivyo hawakazani kujiendeleza.

UKUAJI; huona uwezo wa akili hauna ukomo na hivyo hujiendeleza kwa kujifunza.

2. CHANGAMOTO.

MGANDO; huzikimbia changamoto.

UKUAJI; huzikaribisha changamoto.

3. VIKWAZO.

MGANDO; huona ndiyo mwisho wa safari yao na kukata tamaa.

UKUAJI; huona ni njia ya kufika wanakotaka na hivyo hung’ang’ana.

4. JUHUDI.

MGANDO; huona juhudi hazihitajiki, maana uwezo wao una ukomo.

UKUAJI; huweka juhudi kubwa wakijua zitabadili uwezo wao.

5. KUKOSOLEWA.

MGANDO; huepuka kila aina ya ukosoaji na hawajifunzi.

UKUAJI; hupokea ukosoaji na kujifunza.

6. MAFANIKIO YA WENGINE.

MGANDO; huona wivu pale wengine wanapofanikiwa na kuona ni hatari kwao.

UKUAJI; hufurahia mafanikio ya wengine na kujifunza kutoka kwao.

7. MAFANIKIO.

MGANDO; mafanikio yao hufikia kilele mapema na hawafanyi makubwa.

UKUAJI; wanafikia mafanikio makubwa na kuendelea kufanikiwa zaidi.

Je ungependa kujua uko kwenye mtazamo upi na jinsi ya kuwa na mtazamo sahihi utakaokuwezesha kuwa na maisha bora na ya mafanikio? Karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu cha MINDSET.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hicho pamoja na vingine vingi, jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Mtazamo ulionao unaweza usiujue lakini ukawa kikwazo kikubwa kwako. Soma sasa uchambuzi wa kitabu cha MINDSET ujue ni mtazamo upi ulionao na jinsi ya kuubadilisha.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.