Maisha yana changamoto, hakuna chochote kitakachokwenda kama ulivyopanga kwa asilimia 100.

Utaweka mipango yako vizuri na kuanza kuitekeleza, lakini baadaye utakutana na vikwazo na changamoto ambazo zinakuzuia kupata kile unachotaka.

Hapo ndipo wengi hukwama, kukata tamaa na kuachana na safari waliyokuwa wameianza.

Lakini haipaswi kuwa hivyo, kama kweli umejitoa kupata unachotaka, hakuna kinachoweza kukuzuia usikipate.

Kikwazo kikuu kipo kwenye mtazamo ulionao na tabia ambazo umejijengea.

Mfano kwa wengi, pale wanapokutana na vikwazo au changamoto, wanakimbilia sehemu zisizo sahihi.

Wengi hukimbilia kwenye usumbufu, ili wasahau changamoto zinazowakabili. Na kwa sasa, usumbufu umekuwa rahisi kukimbilia, maana upo karibu yako, kupitia simu janja yako ambapo unaweza kuingia mtandaoni na kuperuzi mambo mbalimbali.

Wengi wanapokutana na changamoto, wanakimbilia kwenye mitandao ya kijamii, ambapo hakuna cha msingi wanakwenda kupata zaidi ya kufuatilia tu maisha ya wengine na kupoteza muda wao.

Wengine wanakimbilia vilevi mbalimbali, wengine vyakula vitabu, wengine tv.

Hatua ya kwanza kwako kuchukua kuanzia sasa ni kubadili wapi unapokimbilia pale unapokutana na vikwazo au changamoto. Badala ya kukimbilia kwenye usumbufu kama ulivyozoea, anza kukimbilia kwenye vitu vitakavyokujenga zaidi.

Na moja ya vitu hivyo ni vitabu, kila unapokutana na ugumu au changamoto na kuona huwezi kuendelea kwa wakati huo, basi soma kitabu. Chagua kitabu kinachoendana na kile unachofanya, kisha kuwa nacho wakati wote. Kila unapokwama na unataka kuacha kufanya kwa muda ili upate kwanza mawazo au mbinu bora, basi kimbilia kwenye kitabu.

Uzuri ni kwamba kwa kila unalofanya au kupitia, kuna wengine walishapitia na wakaandika vitabu. Kwa kila ugumu au changamoto unayopitia, wewe siyo wa kwanza, wengine wengi walishapitia.

Hivyo kwa kuwa mtu wa kusoma vitabu, utapata majibu mazuri kwa changamoto mbalimbali zinazokukabili na kuweza kusonga mbele badala ya kukata tamaa na kuacha.

Madhara ya usumbufu ni haya, unapokwama na kukimbilia kwenye usumbufu, unakuwa rahisi kwako na kile ulichokuwa unafanya kinakuwa kigumu zaidi na zaidi, hivyo huwezi kurudi kukifanya. Hebu fikiria ulikuwa unafanya jukumu gumu, ukashindwa kuendelea, ukasema wacha uingie instagram, huko ni rahisi kuchochea hisia zako na hutataka kurudi tena kwenye jukumu gumu.

Uzuri wa kukimbilia kwenye vitabu, hasa vile ambavyo ni sahihi ni kwamba vinakupa nguvu na hamasa ya kuendelea kufanya kile ulichokua unafanya. Pamoja na magumu uliyokutana nayo, utarudi ukiwa na msukumo mkubwa zaidi.

Chagua aina ya vitabu ambavyo vitakupa msukumo kwenye kile unachofanyia kazi, inaweza kuwa vya wasifu (biography) wa wale waliofanikiwa kwenye eneo hilo au vyenye misingi na mafunzo ya kufanikiwa eneo hilo. Chagua vitabu vichache ambavyo utaambatana navyo wakati wote na kila unapotaka kuondoka kwenye kile unachofanya, kimbilia kwenye vitabu hivyo.

Kuna vitu vingine vinaweza kuonekana vizuri kukimbilia, lakini vinaweza kuwa na madhara, mfano ni kusoma, kusikiliza au kuangalia mafunzo ya hamasa mtandaoni. Ukishaingia tu kwenye mtandao, unakaribisha usumbufu ambao utakuondoa kwenye kile muhimu unachotaka kufanya.

Hivyo kama kuna mafunzo ya hamasa unayofuatilia, yapakue kabisa na uwe nayo kwenye kifaa chako na kama utataka kuyasoma, kuyasikiliza au kuyaangalia, basi isiwe ni mtandaoni moja kwa moja.

Vifanye vitabu sahihi kuwa kimbilio lako na hivyo vitakupa mwongozo sahihi wa kuvuka kila ugumu na changamoto unazokabiliana nazo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha