“If a man sets out to study all the laws, he will have no time left to transgress them.” – Johann Wolfgang von Goethe

Kama lengo lako ni kujua kila kitu ndipo uanze kufanya, kamwe hutafanya.
Maana kuna mengi ya kujua na kila siku mengi zaidi yanazalishwa.

Kama unasubiri uwe na maarifa yote ndiyo uanze kufanya, hutapata muda wa kufanya, maana maarifa yanakuja kama mafuriko.

Tayari unajua kiasi cha kukutosha kuanza kufanya,
Anza sasa kufanya na kama utakutana na vikwazo au changamoto, utarudi kutafuta maarifa ya kukuwezesha kutoka ulipokwama.

Kwa kusubiri mpaka ujue kila kitu ndiyo uanze, unajichelewesha, maana hakuna siku utakayoona umeshajua kila kitu.
Kwa kuanza na kisha kuendelea kujifunza kadiri unavyokwenda, unapata nafasi ya kupiga hatua, huku pia ukijifunza yale muhimu na unayotumia.

Ukijifunza tu bila kufanya, unapoteza muda wako kujifunza mengi ambayo hutayatumia kabisa.
Lakini ukifanya huku unajifunza, unajifunza yale utakayoyatumia.

Muda wetu ni mchache, nguvu zetu zina ukomo ila maarifa yanaongezeka kila siku.
Ukisema unakimbizana na maarifa mpaka umalize yote, hutapata muda wala nguvu za kufanyia kazi yale unayojifunza.
Badala yake anza kufanya na jifunze kulingana na matokeo unayopata.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu matatizo yanayotatuliwa na fedha, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/09/2109

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani