Asili huwa inajiendesha kwa kanuni zake yenyewe na haijawahi kushindwa kwenye hilo. Kila kitu kinaenda kwa taratibu zake na asili haina uonevu wala upendeleo.

Asili haina wema wala ubaya, bali inaenda kwa namna ambayo ni bora kwa asili kwa ujumla.

Simba kumla swala inaweza kuonekana ni uonevu kwa swala, lakini bila kula swala simba hataweza kuishi na simba wasipokuwepo swala watakuwa wengi kiasi kwamba watamaliza rasilimali nyingi za asili, wao wenyewe watashindwa kuendelea na maisha na hatimaye kufa kwa njaa.

Uwepo wa simba unawafanya swala wawe kwenye kiwango fulani. Simba nao wakizidi swala wataisha na hapo simba watakosa chakula na kufa kwa njaa.

Huu ni mfano rahisi wa simba na swala, lakini unaweza kuutumia kwenye vitu vingine.

Somo kubwa la kujifunza hapa ni kuna wakati huwa tunajikuta njia panda, tunapaswa kufanya kitu ambacho kitawaumiza wengine, lakini kina manufaa kwa ujumla. Hapo unaweza kuona ni kukosa wema, kuona ni uonevu kwa wengine. Lakini unapoiangalia asili, unajua kwamba vitu vibaya huwa vinatokea na siyo kwa sababu ya uonevu, bali kwa manufaa ya wote.

Unapolazimika kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuwa maumivu kwako au kwa wengine, usijisikie vibaya, bali angalia yale manufaa ya jumla ambayo yanatokana na maamuzi yako na simamia hilo.

Hii ndiyo hupelekea uongozi kuwa mgumu, kiongozi akitaka akubalike na kila mtu ataogopa kufanya maamuzi yanayowaumiza baadhi. Lakini kikubwa zaidi, kiongozi anapokuwa na nia njema kwa kila anachofanya, na kusimamia chenye manufaa kwa wote, hata pale anapofanya maamuzi yenye maumivu bado anaoumia wanampenda na kumkubali, kwa sababu wanajua hakuna namna ya kusonga mbele bila ya maumivu.

Kama asili ingekuwa inasikiliza maoni ya kila mtu, isingeweza kufanya chochote, mmoja anataka mvua, mwingine anataka jua, huyu anataka joto, yule anataka baridi. Asili inachofanya ni kile chenye manufaa kwa wote na hivyo watu wanajiweka kulingana na asili inavyofanya.

Na wewe pia, usitake kumridhisha kila mtu, badala yake kuwa wewe, fanya kile chenye manufaa kwa wengi na kwa kila unachofanya, kuwa na nia njema, usitake kujinufaisha kuliko wengine na usitake kumuumiza yeyote kwa makusudi. Kwa kuzingatia hili, utafanya maamuzi bora kwako na kwa wengine na kuwa kiongozi bora na mwenye mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha