Hakuna uhuru unaopatikana kwa kutegemea wengine, unaweza kuona kuna uhuru kwenye hilo lakini ni swala la muda tu kabla watu hao unaowategemea hawajaja na masharti yao, ambayo yanaweza kuwa kikwazo kwako.
Tuchukue mfano mzuri wa mitandao ya kijamii, wakati inakuja kila mtu alishangilia kwamba sasa mawasiliano yana uhuru kamili. Huhitaji tena kusubiri mpaka ukubaliwe na vyombo vikubwa vya habari au wachapishaji ndiyo mawazo yako yawafikie wengi. Kwa kutumia mitandao ya kijamii, unaweza kufikisha ujumbe wako kwa yeyote dunia nzima bila kikwazo.
Wote tunafurahia na kuingia kwenye mtego huo, tukaiamini mitandao hiyo na kuipa nguvu. Lakini ambacho kimekuja kutokea ni tofauti kabisa na mategemeo yetu.
Cha kwanza ni mitandao imetengeneza ukiritimba, kumekuwa na mitandao mikubwa michache ambayo inazuia mitandao mingine midogo isichipukie, kwa kuinunua na inapokataa basi wanashindana nayo kuhakikisha wanaiua.
Baada ya mitandao kuwa michache na yenye nguvu kubwa, sasa imekuja na masharti yake, kwamba huna tena uhuru wa kuifikia dunia nzima utakavyo. Kitakachoifikia dunia ni kile ambacho mitandao hiyo inaona ni sahihi.
Masharti hayo yapo kwa nia njema, kuhakikisha wachache wenye nguvu na ujumbe mbaya hawatumii mitandao hiyo vibaya. Lakini wote tunajua vitu vyote vinavyofanywa kwa nia njema kwa wengi, huwa vinakuwa kikwazo kwa wachache ambao wana nia njema pia.
Hivyo uhuru tulioutegemea kwenye mitandao hii, umetoweka, sasa nayo imeanza kuwa na ukaguzi na udhibiti kwenye kila kinachopita kwenye mitandao hii, jambo ambalo linazuia mawazo ya tofauti yasipate nafasi ya kuwafikia wengi.
Ujumbe mkuu ninaotaka utoke nao hapa rafiki yangu ni huu, kamwe usihadaiwe na uhuru ambao wengine wanakuambia wanakupa, huwa unakuja na masharti na gharama zake baadaye.
Kama unataka uhuru wa kweli, uhuru ambao hauna masharti basi utengeneze wewe mwenyewe. Endesha maisha yako na kila unachofanya kwa namna ambayo huweki utegemezi mkubwa kwenye mambo ya wengine.
Hili halimanishi kwamba hupaswi kushirikiana na wengine, shirikiana nao kadiri uwezavyo, lakini tu usijidanganye kwamba watu hao wanakupa uhuru kama wanavyoahidi au unavyotegemea.
Tumia kila fursa na kila rasilimali inayokuja mbele yako kwa namna bora kwako, lakini usijidanganye kwamba itakuwa kama ilivyo milele, kila kitu kinabadilika na wale wenye nguvu juu ya kitu fulani wanaweza kuja na masharti ambayo yatakuathiri.
Usianze kulalamika na kusema hukutegemea hilo, umeshajua sasa, chukua hatua sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante Sana kocha Kwa makala hi nzuri.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike
Siko huru,kwa sababu niko chini ya mtu mwingine. Akisema hanilipi mshaara wa mwezi mmoja,tayari kasha niathiri mimi na familia yangu.
Makala hii inatafakarisha.
Asante sana Kocha.
LikeLike
Chukua hatua kujikomboa na kuwa huru.
LikeLike