Matatizo mengi katika mahusiano huwa yanasababishwa na wahusika wenyewe. Walioko kwenye mahusiano wanatengeneza matatizo yanayokuja kuwaumiza wao wenyewe.
Watu wengi walioko kwenye mahusiano wanayaendesha mahusiano yao kwa hisia na siyo kwa kutumia akili. Kwa mfano, mtu akitaka kuingia kwenye maisha ya ndoa, anamtafuta mwenza wake kwa hisia na wala siyo akili. Na baadaye matatizo yanapokuja ndiyo anakuja kuhalalisha maamuzi aliyofanya kwa akili.
Wengi kwenye mahusiano wapo hivyo, wanafanya maamuzi kwa hisia halafu baadaye mambo yakija kwenda ndivyo sivyo wanatumia sasa akili kuhalalisha kama kile alichofanya ni sahihi au siyo sahihi.
Kama wanandoa wengi wangekuwa wanakubali kuongozwa na akili basi, tungepunguza idadi ya matatizo.
Kila mwanandoa ana matatizo yake. Hivyo kuna wakati unatakiwa usikubali kuumizwa na matatizo ya mwenzako maana matatizo uliyokuwa nayo tayari yanakutosha sasa ukiongeza na matatizo ya mwenza wako utakuwaje?
Njia rahisi ya kuepuka kuumizwa na mwenzako ni kupuuzia yale anayokufanyia. Huenda anafanya hivyo anavyofanya kwa sababu ndiyo hisia zake zinavyomtuma kufanya hivyo na yeye anaona ni sawa kufanya hivyo, huku wewe ukiona siyo sawa na unaendelea kuumia.
Ukiwa ni mtu wa kukasirika kwenye ndoa utapoteza maisha yako mapema. Misongo ya mawazo itaweza kukumaliza kabla hata ya muda wako.
Huwezi kumbadilisha mtu uliyekutana naye ukubwani awe kama vile unavyotaka wewe kwani hayo ni mambo ambayo yako nje ya uwezo wako. Na kadiri unavyokazana kumbadilisha ndiyo anazidisha kile ambacho wewe hukitaki kutoka kwake.
Jifunze kupotezea siyo kila kitu unaruhusu kikutibue. Siyo kwamba matatizo ya ndoa yanawaumiza watu hapana, bali mitazamo ya watu waliyonayo katika ndoa ndiyo inawasumbua. Kiasili ndoa haina shida, ila wanandoa ndiyo wenye shida.
Hakuna kitu kinachowasumbua watu katika ndoa. Ila namna wanavyotafsiri changamoto wanazokutana nazo.
Falsafa ya ustoa inasema kuwa, matukio hayawasumbui watu ila watu wanavyohukumu hayo matukio ndiyo yanapelekea yawaumize. Kwa jinsi wanavyoyachukulia mambo kwa mtazamo na hisia zinazowaumiza.
Kifupi ni kwamba kinachokusumbua siyo kile kinachotokea kwenye ndoa bali namna unavyotafsiri yale yanayotokea.
Anayekusumbua si mwenza wako, bali namna unavyotafsiri yale anayokufanyia mwenza wako.
Msababishi mkubwa wa matatizo ya ndoa yako ni wewe mwenyewe. Umekubali matatizo yakusumbue badala ya kuyapotezea.
Pale mwenza wako anapokufanyia vitu ambavyo hujapendezwa navyo jifunze kumpotezea. Maana ukisema ukasirike kwa kila jambo utakuwa ni mtu wa kukasirika tu. Mchukulie mwenza wako ni kama mtoto pale anapokuudhi, tena ikiwezekana cheka na endelea na maisha yako. Usikubali kuumizwa hata siku moja maana wewe ndiyo unayechagua kuumizwa au l hakuna anayeweza kutoa idhini hiyo bila ya wewe kuruhusu.
Hatua ya kuchukua leo; usikubali kujiumiza kwa matatizo ya mwenza wako. Mchukulie mwenza kama vile ni mtoto pale anapokuudhi maana matatizo uliyonayo tayari yanakutosha acha kujiongezea.
Mwisho, jifunze kumwelewa mwenza wako na wakati mwingine usiwe mtu wa kukasirika sana. Jifunze kupuuzia mambo mengine ili uweze kuishi kwa amani maana ukisema ukasirike kwa kila jambo utakuwa ni mtu wa kujiumiza kila siku. Hujaja duniani kuwa bingwa wa kuvumilia matatizo bali kufurahia maisha sasa ukiwa mtu wa kukasirika kwenye kila jambo utaweza kuyafurahia maisha yako?
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu nakwenyeklabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl. Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana