Kila unapoendelea kusubiri na usianze kufanya kile ulichopanga kufanya, kuna gharama ya zaidi ambayo utalazimika kuilipa.

Kila unaposubiri mpaka tarehe ya mwisho ya kufanya kitu ikaribie ndiyo ufanye, utakifanya kwa haraka na ubora utakuwa hafifu kitu ambacho kitakugharimu zaidi au kukupunguzia manufaa ambayo ungeyapata kama ungekifanya mapema.

Kila unaposubiri mpaka usukumwe na wengine ndiyo ufanye kile unachopaswa kufanya, kuna gharama ya ziada utakayolazimika kuilipa. Utafanya kwa kuwaridhisha wanaokusukuma na hutafanya kwa ubora na hilo halitakunufaisha.

Kila unaposubiri mpaka uone wengine wanafanya ndiyo na wewe ufanye, kuna gharama kubwa utailipa, utajiingiza kwenye ushindani mkali ambao utasababisha utawanye rasilimali zako kukabiliana nao badala ya kuweka rasilimali zote kwenye kile unachofanya.

Jikumbushe hili kila wakati kwenye mipango unayojiwekea, kadiri unavyoanza mapema ndivyo gharama kwako inakuwa ndogo. Kadiri unavyosubiri kuanza, ndivyo gharama kwako inakuwa kubwa.

Jua kile unachotaka, panga jinsi ya kukipata na anza mara moja kutekeleza mipango ya kukipata. Chagua kulipa gharama kidogo kwa kuanza mara moja, au kulipa gharama kubwa baadaye kwa kutokuanza mara moja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha