“As your island of knowledge grows, so too does the shoreline of ignorance.” – John Wheeler

Watu wengi hufikiri lengo la kujifunza ni kujua kila kitu.
Kabla hawajaanza kujifunza, huamini wanajua karibu kila kitu.
Hivyo wanapoingia kwenye kujifunza, hasa kwa kujisomea vitabu ndiyo wanakutana na ukweli ambao hawajawahi kuujua.
Kadiri kisiwa cha maarifa aliyonayo mtu kinakua kikubwa, ndivyo pia ufukwe wa ujinga wake unavyozidi kuwa mkubwa.

Kwa lugha rahisi ni kwamba kabla hujaanza kujifunza unajiona unajua mengi.
Lakini unapoanza kujifunza ndipo unajua kwamba kuna mengi mno huyajui.
Unasoma kitabu kimoja na ndani yake kuna vitabu vingine vilivyotajwa na vya rejea zaidi ya 10.
Unajifunza dhana moja unakuta imeungana na dhana nyingine nyingi ambazo huzijui.

Wengi wanapojikuta kwenye hali hii huwa wanakata tamaa.
Wanaona haina maana kuendelea kujifunza.
Wapo wanaochagua wajifunze vitu vichache tu na kuachana na vingine vingi.
Lakini hilo halitasaidia, kujificha kutokujua hakubadili hali yako.
Badala yake unapaswa kuendelea kujifunza na kukubali yale usiyojua na kama ni muhimu kupanga kujifunza.
Usitake kujua kila kitu, usitake kusoma vitabu vyote, bali wewe jua kipi muhimu kwako na ujifunze hicho.

Asubuhi ya leo tafakari ni vitu gani muhimu kwako, unavyofanyia kazi kila siku kwenye kazi, biashara na maisha yako na hujavijua kwa undani. Tenga muda ambao utakuwa unajifunza vitu hivyo, huku ukijua kadiri unavyojifunza ndiyo utaona mengi ambayo huyajui.
Katika hayo, chagua yale muhimu zaidi na endelea kujifunza hivyo.
Kila siku ni ya kujifunza, weka vipaumbele kwenye yale mengi usiyoyajua na jifunze.
Kujua usiyojua ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye hekima,
Maana mtu mwenye hekima sana kuwahi kuwepo hapa duniani, Socrates aliwahi kusema najua kitu kimoja kwa uhakika, kwamba kuna mengi ambayo siyajui.
Sasa wewe unawezaje kupata ujasiri wa kuamini unajua kila kitu?

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kutafuniwa, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/22/2122

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.