Kuna kitu kimoja muhimu sana unachopaswa kuelewa kwenye safari ya maisha na mafanikio.
Unaweza kupata kile unachotaka au kufika kule unakotaka kufika, lakini maisha hayataenda kama unavyotaka wewe yaende.
Kupata unachotaka na maisha kwenda vile unavyotaka wewe ni vitu viwili tofauti kabisa.
Na kutokujua tofauti hiyo kumekuwa kikwazo kwa wengi kupata wanachotaka au kufika wanakotaka kufika.
Kwa sababu wanataka maisha yaende kama wao wanavyotaka, yasipoenda hivyo wanakata tamaa na hilo linawazuia wasipate wanachotaka.
Chukua mfano una safari ya kutoka Dar es salaam kwenda Arusha, inabidi usafiri siku hiyo lakini unafika kituo cha mabasi na kukuta mabasi ya Arusha yote yamejaa. Kwa wengi wataona hakuna tena safari, maana ulitaka ufike kituo cha basi upate basi la Arusha na kusafiri. Lakini kwa anayetaka kusafiri kweli, ambaye anataka kufika Arusha siku hiyo, ataona mabasi ya Arusha hakuna, lakini atauliza kuna mabasi ya wapi, atajua kuna mabasi ya Tanga na hapo atapanda kwenda Tanga na akifika Tanga atatafuta usafiri wa Arusha.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako, angalia picha kubwa ya mbele, angalia maono yako makubwa na kwa kila unalopitia, angalia ni jinsi gani linakufikisha pale. Inawezekana mambo yasiende kama ulivyopanga, lakini haimaanishi ndiyo mwisho wa safari.
Mara zote angalia pale ulipo na unapatumiaje kufika kule unakotaka kufika. Kitu chochote kisiwe kikwazo kwako, kama bado uko hai, nafasi ya kufika unakotaka kufika ipo, ni wewe kutumia pale ulipo sasa kufika huko.
Maisha hayataenda kama unavyotaka yaende, lakini hilo siyo kikwazo kwako kufika kule unakotaka kufika na kupata unachotaka kupata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,