“Those who do not think independently are under the influence of somebody else who thinks for them. If you give your thoughts to somebody else, it is a m ore shameful slavery than if you give your body to someone to possess.” – Leo Tolstoy
Kila mtu anafurahia kwamba biashara ya utumwa imefutwa duniani.
Kwamba hakuna tena mtu anayewamiliki watu na kuwatumikisha anavyotaka yeye mwenyewe.
Lakini je hilo ni kweli?
Siyo kweli kwamba utumwa umeisha, bali umebadilika.
Utumwa wa kimwili umeondoka ila kwa sasa kuna utumwa mbaya zaidi ambao ni wa kifikra.
Utumwa huu ni mbaya kwa sababu hakuna anayejua anatumikishwa.
Unajiamini kwamba umefanya maamuzi yako mwenyewe, kumbe kuna watu wamekuseti ili ufanye maamuzi ya aina hiyo.
Kila mtu anawinda fikra zako na umakini wako.
Vyombo vya habari, matangazo mbalimbali na hata mitandao ya kijamii, vyote vimejengwa kwa namna ya kuathiri fikra zako bila kujua.
Uhuru kamili unaoweza kuwa nao zama hizi ni kuhakikisha unafikiri mwenyewe na kufanya maamuzi yako mwenyewe.
Epuka sana ushawishi ambao wengine wanaleta kwako, ili ufikiri wanavyotaka wao na ufanye maamuzi yanayowanufaisha wao.
Asubuhi ya leo tafakari maamuzi mengi ambayo umekuwa unayafanya na jiulize kama ni fikra zako au ushawishi wa wengine.
Kuanzia imani ulizonazo, vitu unavyopendelea, manunuzi unayofanya na hata wale unaowakubali au usiowakubali.
Je ulikaa chini na kufikiri wewe mwenyewe kisha kufikia maamuzi hayo au ulishawishiwa na wengine?
Kwa mambo yote muhimu kwenye maisha yako, hakikisha unafikiri mwenyewe na kufikia maamuzi mwenyewe.
Utumwa wa kifikra ni mbaya kuliko hata wa kimwili,
Watu wengi sasa wanatumikishwa na utumwa huu bila ya wao kujua.
Wewe kuwa makini, usikubali kutumikishwa kifikra.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu hamsini kwa hamsini, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/28/2128
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.