Watu huwa wanasema muda ni pesa, lakini kauli hiyo siyo sahihi, muda siyo sawa na pesa, muda ni zaidi ya pesa. Na sababu moja ya msingi kabisa ni kwamba ukipoteza pesa unaweza kupata nyingine, lakini ukipoteza muda huwezi kuupata tena, ndiyo umepotea moja kwa moja.
Hivyo kati ya muda na pesa, unapaswa kujali zaidi muda kuliko pesa. Ila cha kushangaza wengi wanafanya kinyume, wanajali pesa kuliko muda na kinachotokea ni wanakosa vyote.
Watu wengi wamekuwa wanakazana kutumia muda ili kuokoa pesa badala ya kutumia pesa ili kuokoa muda.
Chukua mfano una majani ya kufyeka kwenye nyumba yako, zoezi ambalo litakuchukua siyo chini ya saa moja. Unapata wazo la kumpa mtu kazi ya kuyafyeka, anakuambia umlipe elfu kumi. Wewe unajiambia elfu kumi yote hiyo, acha niyafyeke mwenyewe. Unatumia muda wako ili uokoe pesa.
Hilo halikusaidii, kwa sababu kazi yako kuu kwenye maisha siyo kufyeka majani, bali ni kazi au biashara nyingine unayofanya. Kutumia saa moja kufyeka majani ni muda ambao huwezi kuutumia kwenye kazi au biashara yako. Hivyo unaona unaokoa pesa, lakini unapoteza zaidi.
Ambacho ungepaswa kufanya kwenye mfano huu ni kujiuliza ni kitu gani unaweza kufanya kwenye kazi au biashara yako kwa saa moja na ukaingiza mara mbili ya kile kiasi unachomlipa wa kukusaidia kufyeka majani. Kama anataka umlipe elfu kumi, jiulize huo muda unaookoa unawezaje kuutumia kuingiza elfu 20, kisha fanya hilo.
Hii inaweza kuwa njia nzuri sana kwako kukusukuma kuingiza kipato. Kwa kila shughuli binafsi unayoifanya ambayo haihusiani na kazi au biashara yako kuu, tathmini ni muda kiasi gani kwa siku, wiki na mwezi unatumia kwenye shughuli hizo. Kisha piga mahesabu kama ungewapa watu wafanya shughuli hizo wangekugharimu kiasi gani. Ukishapata hiyo namba, zidisha mara mbili, kisha jiulize kwa muda utakaookoa kufanya shughuli hizo, ni vitu gani unaweza kufanya kwenye kazi na biashara yako na ukazalisha mara mbili.
Hii pia unaweza kuitumia kwenye maamuzi ya kuajiri msaidizi binafsi. Watu wengi hawajui ni wakati gani wanapaswa kuajiri msaidizi binafsi, mtu ambaye atafanya majukumu madogo madogo ambayo ungepaswa wewe uyafanye, lakini yanachukua muda wako mwingi. Orodhesha majukumu yote na muda unaotumia, kisha pima gharama utakayomlipa msaidizi binafsi na jinsi unavyoweza kutumia muda huo kupata mara mbili ya kile unachomlipa. Hilo litakusukuma kutumia muda wako vizuri na kuongeza kipato zaidi.
Usihangaike kutumia muda ili kuokoa pesa, badala yake hangaika kutumia pesa ili kuokoa muda. Tambua muda ukishapotea haurudi tena, hivyo ni wa thamani kuliko pesa, linda na tumia vizuri muda wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nitaitumia pesa ili kuokoa muda wangu. Asante sana kocha.
LikeLike
Vizuri Datius
LikeLike