Kwenye fizikia kazi inakuwa imefanyika pale nguvu zinapotumika kusogeza kitu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kwa maana hii, ukisukuma ukuta kama haujaanguka hakuna kazi umefanya, hata kama umetokwa jasho na kuchoka kiasi gani, kwa sababu nguvu uliyoweka haijasogeza ukuta huo kwa namna yoyote ile.
Unaweza kuwa uliisikia dhana hii na kuipuuza, kwa kuwa huna matumizi ya fizikia kwenye maisha yako ya kila siku, lakini leo nataka nikuambie ni dhana moja kubwa na unayopaswa kuitumia kila siku kwenye maisha yako, itakusaidia sana kujua ni hatua zipi unapiga.
Kama unaweka juhudi na hakuna chochote kinachobadilika, kuna tatizo kwenye juhudi unazoweka au kwenye kile ambacho unakiwekea juhudi. Wengi wamekuwa wako ‘bize’ kila siku, miaka nenda, miaka rudi, hakuna matokeo yoyote ya tofauti wanayoyazalisha, lakini hawapati nafasi ya kujua hilo, kwa sababu hawajitathmini na kujipima.
Leo nataka nikushirikishe eneo moja ambalo tumekuwa tunapoteza nguvu huku hakuna kinachobadilika, hivyo tunakuwa hatujafanya kazi yoyote.
Mawazo hasi, huwa yanatumia nguvu ya akili mara mbili zaidi ya mawazo chanya. Lakini mawazo hayo hasi hayakuwezeshi kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako, hivyo licha ya kutumia nguvu zaidi, matokeo ni sifuri, hivyo hakuna kazi inayokuwa imefanyika.
Kwa kutumia kanuni hii ya kifizikia ya kazi, ni wakati sasa wa kuchuja kila wazo linaloingia kwenye akili yako, kabla hujaruhusu litumie nguvu ya akili yako, angalia kwanza lina mchango gani, linakuwezesha kupiga hatua gani. Kama hakuna hatua unazoweza kupiga kwa wazo linalokujia, achana nalo.
Hofu ni moja ya fikra ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi, haijalishi una hofu kiasi gani, hakuna namna unaweza kutumia fikra hizo kupiga hatua zaidi. Hivyo badala ya kuruhusu akili yako izame kwenye fikra za hofu, badili na fikiria ni kitu gani unaweza kufanya kwa ile hali unayohofia. Badala ya kuangalia kila baya linaloweza kutokea, jiulize ni kipi unachoweza kufanya. Kwa kufanya hivyo utapunguza nguvu za akili huku ukiwa unapiga hatua na hivyo kazi kuwa imekamilika.
Hakikisha nguvu zako za akili zinatumika sawa, kwa kuwa na fikra ambazo kuna hatua unaweza kuchukua badala ya fikra ambazo hakuna hatua utakazochukua. Fikra chanya zina hatua za kuchukua huku fikra hasi zikiwa hazina hatua za kuchukua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,