Hayapo,

Huwa siyo mpenzi wa kuangalia tv, lakini ninapojikuta kwenye hali ambayo naangalia tv, basi huwa napendelea kuangalia stesheni inayorusha vipindi vya wanyama. Napenda vipindi hivyo kwa sababu vinaonesha jinsi asili inavyofanya kazi, jinsi viumbe mbalimbali wanavyopangana kuendesha maisha yao katika mazingira ambayo ni magumu lakini wanafanikiwa.

Siku moja nikiwa nimemtembelea rafiki na nikawa namsubiri akiwa anakamilisha kitu fulani, nililazimika kuangalia tv kwa muda na hapo niliomba iwekwe chaneli ya wanyama.

Nilikuta kipindi ambacho kipo katikati, lakini kilikuwa kinalinganisha kiwango cha mafanikio kati ya wanyama wanaowinda, ilikuwa kati ya simba na duma (Cheetah). Ilionesha kwamba duma ana kiwango cha mafanikio cha asilimia 50 mpaka 60 huku simba akiwa na kiwango cha mafanikio cha asilimia 10 mpaka 20. Wakalinganisha na paka pia ambapo paka wa nyumbani kiwango cha mafanikio ni asilimia 30, huku paka mwitu kiwango cha mafanikio kikiwa asilimia 60.

Kuna mengi yaliyoelezwa kuchangia tofauti hiyo ya kiwango cha mafanikio, mfano paka mwitu wana kiwango kikubwa cha mafanikio kwa sababu wanawinda usiku na mchana, huku simba wakiwinda mchana tu.

Nilipoona viwango hivyo vya mafanikio, ilinifikirisha, kwamba pamoja na hatari na ukali wa mnyama kama simba, siyo mara zote anapata anachowinda. Kwa kiwango cha asilimia 20 ya mafanikio ina maana kwamba kwa kila wanyama 10 ambao simba anawawinda, anafanikiwa kukamata wawili tu. Lakini simba ndiye mfalme wa mwitu, ndiyo mnyama anayeogopeka na hujawahi kusikia simba akilia kushindwa au akifa njaa.

Hili lilinifanya nifikirie haya shuleni, kiwango cha ufaulu siyo maksi 100 kwenye mtihani wowote ule, bali ukiweza kuvuka 50 tu, tayari umefaulu.  Hata anayekuwa wa kwanza kwenye mtihani wowote ule, hapati alama 100.

Kumbe kwenye maisha hakuna anayekutegemea upate kila kitu, hakuna anayeweza kupata kila kitu, hata awe nani.

Lakini cha kushangaza ni inapokuja kwenye mipango unayojiwekea, unataka upate kila ulichopanga, kama ulivyopanga, tofauti na hapo unajiona umeshindwa, unajiona hufai.

Hebu fikiria simba ambaye ameianza asubuhi, akamuona swala, akamkimbiza na kumkosa, akaona mnyama mwingine, kamkimbiza na kumkosa, akaona mwingine tena, labda ni watano, lakini wote hajakamata hata mmoja. Je simba huyo atarudi kulala na kujiambia leo ana kisirani au hawezi tena kukamata wanyama kwa kitoweo? Jibu ni hapana, ataendelea kuwinda mpaka akamate mnyama, na huenda mnyama wa sita au wa saba kumkimbiza ndiye atakayemkamata.

Hili ni funzo kubwa sana kwetu inapokuja kwenye safari yetu ya mafanikio, hakuna namna tukapata kila tunachotaka, kwa namna tunavyotaka kupata, lakini hilo halimaanishi kwamba tumeshindwa. Jukumu letu ni kupanga na kuchukua hatua, tunapata nini hiyo haipaswi kuzia kuchukua hatua tulizopanga kuchukua.

Kama ambavyo simba haachi kuwinda kwa sababu mnyama aliyepanga kumwinda mwanzo amemkosa, ndivyo tunavyopaswa kuendelea na mipango yetu hata kama hatujapata kila tunachotaka.

Mafanikio ya asilimia 100 hayapo, hayajawahi kutokea, labda kama ni kwa malengo na mipango ambayo iko chini sana ya uwezo wa mtu. Lakini unapopanga makubwa, basi jua hutapata kwa asilimia 100, lakini hilo halina ubaya wowote, wajibu wako ni kuendelea kuchukua hatua sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha