“We are not satisfied with our real life. We want to live an imaginary life, a life in which we seem different in the eyes of other people than we are in reality.” — Blaise Pascal

Maisha tayari ni magumu kwa kila mtu, bila kujali mtu yupo kwenye hatua ipi ya kimaisha.
Lakini watu wengi wamekuwa wanayafanya kuwa magumu zaidi ya yalivyo, kwa kuishi kwa maigizo.
Wengi wanaacha kuishi uhalisia wao na kuigiza maisha yasiyokuwa yao.
Hilo ndiyo limekuwa linayafanya maisha ya wengi kuwa magumu zaidi.

Asubuhi ya leo tafakari ni kwa namna gani umekuwa unayafanya maisha yako kuwa magumu zaidi, kwa kuigiza maisha.
Kama umewahi kununua kitu chochote usichokitaka, lakini kila mtu anacho, basi jua umeyaigiza maisha, umehangaika kupata usichokitaka ili uwe kama wengine.
Kama umewahi kukopa fedha kwa ajili ya matumizi jua umeyaigiza maisha, kwa sababu umekuwa na matumizi makubwa kuliko uwezo wako.

Usikubali kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi ya yalivyo sasa,
Acha kabisa kuishi maisha ya maigizo,
Ishi maisha halisi kwako, usihofie kwamba wengine watakuchukuliaje, hakuna anayekosa usingizi kwa kufikiria wewe.
Kila mtu anapambana na maisha yako, kila mtu ana magumu na changamoto nyingi zinazoendelea kwenye maisha yake, hayo yanamtinga zaidi na hana muda wa kufikiria mambo yako.

Kuwa huru kuyaishi maisha yako kwa uhalisia, chagua kuwa wewe, utapunguza kuyafanya maisha kuwa magumu na hilo litakuwezesha kupiga hatua na kufanikiwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu nguvu mara mbili, matokeo sifuri, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/01/2132

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.