Utumwa hauwezi kuisha duniani, kila mtu ni mtumwa wa kitu fulani, iwe anajua au hajui. Ule utumwa wa kulazimishwa umeisha, ila utumwa wa kujitakia haujaisha.
Kuna watu ambao ni watumwa wa pesa, wengine watumwa wa mapenzi, huku wengine wakiwa watumwa wa kazi zao na wengine wakiwa watumwa wa dini na itikadi mbalimbali.
Kile ambacho mtu anakikubali pamoja na kuwa na changamoto au madhaifu yake, anageuka kuwa mtumwa wa kitu hicho.
Utumwa unakuwa mbaya pale unapokuumiza bila ya kukupa manufaa yoyote. Wengi wamekuwa watumwa sasa bila ya kujua, huku wakiumia bila ya kujua.
Epictetus, aliyekuwa mwanafalsafa wa Ustoa alizaliwa kwenye utumwa, enzi hizo watu walikuwa wakimiliki watumwa kwa matumizi yao binafsi. Naye alikuwa mmoja wa watumwa, aliyemilikiwa na watu kama mali.
Lakini Epictetus alifanikiwa kuondoka kwenye utumwa huo, na kuchagua utumwa mwingine ambao alitumia muda mwingi kuwashawishi wengine pia wajiunge na utumwa huo mpya. Hiyo ni kwa sababu utumwa huo mpya ulikuwa na manufaa kwake kuliko utumwa aliokuwa awali.
Utumwa mpya kwa Epictetus ulikuwa falsafa, baada ya kujifunza na kuishi kwa misingi ya falsafa, aliweza kuwa huru huku akiyaendesha maisha yake vizuri. Ni manufaa hayo ndiyo yalimfanya Epictetus kumshauri kila mtu awe mtumwa wa falsafa.
Kwa kuwa mtumwa wa falsafa, unayaendesha maisha yako kwa misingi fulani, ambayo umeichagua mwenyewe na hakuna anayekulazimisha, unakuwa umechagua misingi hiyo kwa sababu inakupa manufaa fulani. Labda utulivu wa ndani, uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuboresha mahusiano yako na wengine.
Mengine ambayo Epictetus ametufundisha kupitia utumwa wa falsafa na yenye manufaa ni kama ifuatavyo;
- Tangua mambo yaliyo ndani ya uwezo wako na yaliyo nje ya uwezo wako, hangaika na yaliyo ndani ya uwezo wako na achana na yaliyo ndani ya uwezo wako. Hebu fikiria, kwa hili tu unapunguza changamoto nyingi unazohangaika nazo kwenye maisha yako sasa.
- Usiwe mtu wa kukosoa watu wengine, hujui sababu gani zimewasukuma kufanya kile wanachofanya.
- Usiwe mtu wa kukimbilia kuwasifia wengine kwa yale unayoyaona nje, hujui kilicho ndani yao au watakachokuja kufanya baadaye.
- Usiwe mtu wa kuwalaumu wengine kwa chochote walichokufanyia au kushindwa kufanya. Tambua kila mtu anafanya au kutokufanya kitu kwa nia ambayo kwake anaona ni njema.
- Usiwe mtu wa kuwahukumu wengine, kuna mengi hujui kuhusu wao, ungekuwa kwenye nafasi walizopo huenda na wewe ungefanya kama walivyofanya.
Utaona mengi tunayojifunza hapa ni kupeleka tafsiri zetu binafsi kwa wengine, kitu ambacho ni chanzo kikubwa cha migogoro na kutokuelewana baina ya watu. Ukiweza kuvuka hilo, mahusiano yako na wengine na maisha yako kwa ujumla yatakuwa bora.
Chagua kuwa mtumwa wa falsafa, chagua falsafa inayoendana na wewe na iishi misingi yake. Wengine kwa nje wataona unajitesa lakini kwako unajua nini unafanya na kwa nini unafanya. Pia falsafa hiyo ikusaidie kuacha kuhukumu maisha ya wengine, hujui mengi kuhusu wao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,