“The more urgently you want to speak, the more likely it is that you will say something foolish.” – Leo Tolstoy
Kadiri unavyokimbilia kuongea, ndivyo kile unachoongea kinavyozidi kuwa cha kijinga.
Unapokimbilia kuongea hupati muda wa kutosha kutafakari kitu kabla ya kukisema.
Wengi huishia kujidhalilisha kwa yale wanayokimbilia kuongea.
Wanasema mpumbavu akikaa kimya huwa anaonekana ni mtu mwenye hekima.
Wengi wanajidhalilisha kwa yale wanayokimbilia kusema.
Na kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, unapokimbilia kuandika au kuweka chochote mtandaoni, ndivyo unavyoweka kitu cha kijinga na kinachokudhalilisha.
Asubuhi ya leo tafakari ni mara ngapi umepoteza heshima yako au uaminifu ambao watu walikuwa nao kwako kwa sababu ya kuongea kitu cha kijinga.
Mara zote utaona ulikimbilia kuongea, au kujibu kitu kabla hujafikiria kwa kina.
Kuanzia sasa kuwa makini kabla ya kuongea, kujibu au kuweka chochote mtandaoni.
Kuwa msikilizaji mzuri na uwaelewe wengine kabla hujakimbilia kusema au kujibu.
Kabla ya kusema chochote kwa wengine, jiambie kwanza ndani yako na ujisikilize, uone kama ungesikia kwa mwingine ungechukuliaje.
Kama kuna ujumbe au picha unataka kuweka mtandaoni au kutuma kwa mwingine, usifanye haraka, badala yake jipe muda kidogo.
Sisi ni binadamu, viumbe tunaoendeshwa na hisia zaidi kuliko fikra.
Pale hisia zetu zinapokuwa juu, huwa tunasukumwa kufanya jambo fulani, na mara nyingi jambo hilo huwa siyo sahihi.
Epuka udhaifu huu ambao kila mmoja wetu anao kwa kuhakikisha unajichelewesha zaidi pale hisia zinapokuwa juu.
Neno likishakutoka huwezi kulirudisha mdomoni,
Ukishaweka kitu mtandaoni, hata ukikifuta mtandao huwa hausahau.
Unaweza kujenga sifa yako kwa miaka 10 ukaja kuipoteza kwa sekunde 10 kwa kitu ulichokimbilia kuongea au kuweka mtandaoni.
Hivyo kuwa makini mno kwa maneno yako na yale unayoweka mitandaoni.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu masaa ya kazi na kazi uliyofanya, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/04/2135
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.