Unapoona watu wanafanya mambo ambayo kwako yanaonekana ni ya kijinga, lakini yanawanufaisha, unapaswa ujifunze kutoka kwa watu hao.
Kiburi na ujuaji imekuwa kikwazo kwa wengi kujifunza. Kuchagua upande fulani na kung’ang’ana nao kumewazuia wengi kutokuona ukweli na kuutumia vizuri.
Kulinda kile walichofanya jana na kuwa na msimamo wa kijinga kumewazuia wengi kubadilika na hivyo kushindwa kutumia fursa nzuri zinazokuja mbele yao.
Iko hivi rafiki, kama kuna watu wanaopata matokeo ya tofauti na unayopata wewe, kuna vitu vya tofauti wanavyojua ambavyo wewe hujui. Haidhuru kama utachukua hatua ya kujifunza kupitia wao na kuona wewe unakwama wapi.
Kumekuwa na tabia ya watu kujipa sababu za kujibembeleza, kwamba wale wanaopata matokeo ya tofauti labda wamepata upendeleo au bahati fulani ambayo wao hawajapata.
Lakini huo siyo ukweli, upendeleo na bahati vipo kwa kila mtu, huwa vinatofautiana tu. Kuna mengi ya kujifunza kwa wengine ambayo ukiyafanyia kazi utaweza kupiga hatua kubwa.
Hata kama hukubaliani na wale waliopiga hatua kuliko wewe kimtazamo, kiimani au kiitikadi, kama wamekuzidi kuna kitu kilicho sahihi wanachofanya ambacho wewe hujui au hufanyi.
Weka huu kuwa utaratibu wako, kwa kila mtu unayekutana naye ambaye amepiga hatua kubwa kuliko wewe kwenye kile unachofanya au unachotafuta, kuwa mnyenyekevu na jifunze ni kipi anajua na kufanya ambacho wewe hujui au hufanyi.
Usiwe mtu wa kujipa sababu wala kutafuta cha kukosoa, badala yake jifunze. Ndiyo mtu huyo hatakuwa mkamilifu, atakuwa na madhaifu na makosa yake, lakini kuna kitu cha kujifunza kwake. Wanasema hata saa (ya mshale) mbovu huwa inasema muda sahihi mara mbili kwa siku. Kwa yeyote aliyeweza kupiga hatua fulani kwenye maisha yake, kuna kitu cha tofauti anajua na kufanya, jifunze kutoka kwa watu hao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,