“There is only one you for all time. Fearlessly be yourself.” – Anthony Rapp

“There’s only one success… to be able to live your life your own way.” – Christopher Morley

Miti mingi mno imekatwa ili kuzalisha karatasi za kuchapa vitabu vya siri za watu waliofanikiwa.
Kuna vitabu zaidi ya elfu 2 vinavyoeleza siri za mafanikio ya Warren Buffett kwenye uwekezaji.
Vingine vingi mno kuwahusu mabilionea wengine na wale waliofanikiwa sana.
Lakini dunia imezalisha kina Warren Buffett na Bill Gates wangapi?

Jibu ni sifuri.
Pamoja na siri zao kuelezwa kwenye vitabu, pamoja na watu kujaribu kuwa kama wao, hakuna yeyote ambaye ameweza kuwa kama wao.

Hii ndiyo changamoto kubwa ya hadithi na siri za mafanikio.
Watu wamekuwa wanazitumia kwa namna isiyo sahihi, ndiyo maana hawafanikiwi.

Leo mtu anasoma siri za watu waliofanikiwa ni kuamka mapema, anaanza kuamka mapema
Kesho anakutana na maarifa mengine kwamba waliofanikiwa wanachelewa kulala. Anaanza kuchelewa kulala, hilo linavuruga uamkaji wake mapema na hata siku yake nzima.

Mtu anasoma waliofanikiwa walianza kidogo, kwa kujiwekea akiba zao na kisha kutumia akiba hizo kuanza biashara au uwekezaji, wakaukuza kidogo kidogo mpaka kufakiwa. Anaanza kujiwekea akiba.
Siku nyingine anasoma kwamba waliofanikiwa wametumia pesa za wengine kufikia mafanikio, kwa kuchukua mikopo. Maarifa hayo yanamsisitiza kwamba hakuna utajiri hila mikopo, anakimbilia kukopa na baadaye mkopo huo unamrudisha nyuma.

Mafanikio ya kweli kwenye maisha ni kukazana kuwa wewe,
Kwa sababu kuna wewe wa aina moja tu hapa duniani.
Huwezi kuwa Bill Gates, huwezi kuwa Bakhresa na wala huwezi kuwa Dangote.
Ila unaweza kuwa wewe, hivyo chagua kuwa wewe bila ya kuhofia chochote.
Unaposoma hadithi na siri za mafanikio ya wengine, zitumie kujifunza misingi sahihi ambayo utaitumia kukusaidia kuwa wewe ambaye ni bora zaidi.
Kama unajifunza siri na hadithi za mafanikio ya wengine na kutaka kuwa kama wao, hakuna ulichojifunza na hutaweza kufanikiwa.

Ndiyo maana hatua ya kwanza na ya muhimu kabisa kwenye mafanikio ni kukitambua kwanza wewe mwenyewe.
Ukishajitambua, kwa kujua unataka nini na nini kipo ndani yako, kupitia wengine utajifunza jinsi ya kuwa wewe bora zaidi na siyo jinsi ya kuwa kama wao.

Chagua kuwa wewe bila ya kuhofia chochote, kwa sababu hakuna kama wewe. Waepuke wale wanaokuambiwa unapaswa kuwa namna fulani, hawajui kilicho ndani yako.
Acha kuiga na kujilinganisha na wengine, huna walichonacho na hawana ulichonacho.
Kuwa wewe, kwa sababu ndiyo toleo pekee lililopo na ndiyo mafanikio ya kweli kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kuchagua utumwa wenye manufaa kwako, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/05/2136

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.