“Everyone thinks of changing the world, but no one thinks of changing himself.” — Leo Tolstoy
Kila mtu anafikiria kuibadili dunia na kuifanya kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi. Kitu ambacho kipo nje ya uwezo wa kila mtu, maana dunia haiendi kulingana na matakwa ya yeyote, bali inajiendesha kwa misingi yake yenyewe.
Kila mtu anafikiria kuwabadili watu wengine ili aweze kwenda nao vizuri kwenye mahusiano.
Lakini hilo linashindikana kwa sababu hakuna anayetaka kubadilishwa, kila mtu anataka kuyaishi maisha yake atakavyo yeye. Na kama ni kubadilika basi achague kufanya hivyo mwenyewe na siyo kulazimishwa.
Je hii ina maana kwamba hatuwezi kabisa kuleta mabadiliko hapa duniani na hata kwa wengine?
Tunaweza sana, ila siyo kwa kukazana kuibadili dunia na kuwabadili wengine, ila kwa kuchagua kubadilika sisi wenyewe.
Unapochagua kubadilika wewe, dunia inabadilika na wale wanaokuzunguka pia wanabadilika.
Hiyo inakuwa rahisi kwako kwa sababu unabadilika wewe na siyo wengine.
Njia rahisi na ya uhakika kwako kuibadili dunia na kuwabadili wengine ni kuanza kubadilika wewe mwenyewe.
Tafakari ni mara ngapi umekazana kuibadili dunia na hata watu wengine na jiulize ni matokeo gani umekuwa unayapata.
Acha kupoteza nguvu zako kubadili dunia na wengine, tumia nguvu hizo kujibadili mwenyewe, kukazana kuwa bora na utakapobadilika, dunia na wanaokuzunguka pia watabadilika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu wanachojua wengine ambacho wewe hujui, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/06/2137
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.