Kama unataka kulala, huwezi kutumia nguvu kutafuta usingizi. Ukiingia kitandani kwa kujiambia unakwenda kutafuta usingizi kwa nguvu, hutaupata kabisa. Lakini unapoingia kitandani ukiwa umejiachia kwamba unapumzika, usingizi unakuja wenyewe.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye furaha na mapenzi, huwezi kulazimisha, ukitumia nguvu ndivyo unavyozidi kupoteza vitu hivyo.

Tukianza na furaha, kama unatumia nguvu nyingi kupata furaha, ndivyo unavyozidi kuwa mbali nayo. Kama kila wakati unajiuliza kama una furaha, ndivyo unavyoona jinsi usivyokuwa na furaha. Unapofanya kitu kwa lengo la kupata furaha, ndivyo unavyozidi kuwa mbali na furaha. Unapoiga yale ambayo unaona wenye furaha wanayafanya, unaishia kutokuipata.

Kama ilivyo kwa usingizi, furaha huwa ni matokeo ya vitu vingine unavyofanya, lakini siyo kwa lengo la furaha. Mfano unapoyatoa maisha yako kufanya kitu ambacho ni kikubwa na chenye manufaa kwa wengine, matokeo unayoyazalisha yanakufanya uwe na furaha. Unapokuwa mwema kwa wengine na wao wakakuthamini kwenye hilo, ndivyo unavyokuwa na furaha zaidi. Furaha hizo zinakuja kama matokeo na siyo pale unapoweka lengo la kupata furaha kupitia hayo.

Kadhalika kwenye mapenzi, huwezi kuwalazimisha watu wakupende na wala huwezi kujilazimisha kupenda watu. Kadiri unavyotumia nguvu kwenye mapenzi ndivyo unavyoyakosa. Njia pekee ya kuwa kwenye mapenzi na kupata upendo wa kweli ni kujiachia kwa wengine na kwa kile unachofanya. Kujiachia bila ya kuwa na sababu yoyote, kuwakubali watu kama walivyo, bila ya kutaka wabadilike kwa namna yoyote ile.

Watu wamekuwa na changamoto kwenye mahusiano mbalimbali kwa sababu wanalazimisha mapenzi na upendo. Mtu anasema wazi anampenda mwingine lakini anamtaka awe tofauti, hapo hakuna upendo. Upendo haulazimishwi, bali upendo unatolea na kupokelewa. Ukijikuta unalazimisha upendo, kuna tatizo mahali na huwezi kuupata.

Kuna vitu vingi tunatumia nguvu kwenye maisha, wakati kinachotakiwa ni kujiachia na kutoa au kupokea kadiri watu na mambo yalivyo. Furaha na mapenzi ni moja ya vitu hivyo, tujifunze kuacha kutumia nguvu ili tuweze kunufaika na vitu hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha