“To live the best life,” the Oracle told Zeno, “you should have conversations with the dead.”
Kama unataka kuwa na maisha bora, unapaswa kuongea na wafu.
Na hapa siyo kwa kufanya matambiko, bali kwa kusoma maarifa yaliyoachwa na wale waliotutangulia hapa duniani miaka mingi iliyopita.
Wanafalsafa na waandishi mbalimbali waliweka ujuzi na uzoefu wao wa maisha kwenye maandishi.
Mambo hayo yana msaada mkubwa kwetu hata sasa.
Kama tunavyojua, hakuna kitu kipya hapa duniani, mambo ni yale yale na yamekuwa yanajirudia.
Changamoto yoyote inayokusumbua sasa, ugumu wowote unaokutana nao, jua wewe siyo mtu wa kwanza kupitia hilo.
Kuna wengine wengi walishapitia kile unachopitia, wakaweza kutatua na kubuka na kwa bahati nzuri sana, wakaandika jinsi walivyoweza kuvuka hilo.
Hivyo badala ya wewe kuanza kujaribu namna ya kuondoka hapo ulipo, fanya mazungumzo na wale ambao wamewahi kupitia hilo, kwa kusoma kazi zao mbalimbali na utajua njia sahihi ya kukabiliana na hilo.
Tunayafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa sababu tunataka kufanya kila kitu wenyewe.
Pamoja na maarifa mengi yaliyoachwa na wengine na yenye msaada kwetu, hatuhangaiki kuyapata.
Kijengee utaratibu wa kuwa na mazungumzo na wafu.
Chagua wanafalsafa au waandishi ambao unapenda maisha yako yawe kama yao au ambao walipitia ugumu ambao unaupitia wewe, kisha soma kazi zao zote.
Utajifunza mengi na utayarahisisha sana maisha yako.
Maana kitu ambacho kimemchukua mtu miaka 10 kujua, wewe utakijua ndani ya muda mfupi kwa kusoma kitabu alichoandika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu madhaifu uchwara, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/07/2138
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.