“I call this life a happy one in which I do one good deed after another, with no intervals between them.” — Marcus Aurelius

Maisha ya furaha ni matokeo ya kuwatendea wengine wema.
Unakuwa na furaha pale unapofanya yaliyo mema kwa wengine, na kurudia kufanya hivyo mara kwa mara.
Haijalishi ukubwa wa kitu ulichofanya, bali nia na namna ulivyokifanya.
Na siyo kufanya mara moja, bali kufanya kila wakati.

Wengi wanahangaika kutafuta furaha kupitia vitu fulani, kuhakikisha wana kila wanachotaka.
Wanaweza kupata vile wanavyotaka, lakini bado hawapati furaha ya kudumu.
Kwa sababu binadamu tuna tabia ya kuzoea vitu, unaweza kuwa unakitamani sana kitu kabla hujawa nacho, ila ukishakipata unakizoea na kukichukulia kawaida.

Hivyo kama unataka furaha ya kudumu kwenye maisha yako, tumia kila fursa unayoipata kuwa na wengine kufanya yaliyo mema.
Kuwa mwema na wajali sana wengine.
Angalia ni kwa namna gani unaweza kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi, hata kama ni kwa kufanya kitu kidogo kabisa.
Kisha fanya, matokeo watakayopata na jinsi watakavyokushukuru na kukubali, itakupa kuridhika na kuwa na furaha kubwa.
Rudia hilo kila wakati, kwa kila mtu anayekuzunguka au unayekutana naye.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu haijawahi kuwa rahisi kwa yeyote hivyo unapaswa kupambana, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/17/2148

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.