Moja ya sababu zinazopelekea mifumo ya kijamaa kushindwa ni kukosekana kwa uwajibikaji kwenye maeneo yanayotumia mfumo huo. Kwa kuwa kila kitu ni mali ya kila mtu, inakuwa vigumu kuwajibisha watu. Mtu anakuwa na uchungu pale kitu kinapokuwa chake, kuliko kinapokuwa cha wengine. Kwa kuwa kwenye mifumo ya ujamaa kila kitu ni cha kila mtu, hakuna mwenye uchungu na chochote.

Hali hii inakwenda hata kwenye maisha yetu binafsi, hata kama hatutumii mifumo ya kijamaa. Pale tunapofanya kitu kuwa cha kila mtu, uwajibikaji unakosekana na hakiwezi kwenda vizuri.

Mfano kama kuna kazi inafanyika na watu wengi, na hakuna mmoja anayeweza kuwajibishwa kwa matokeo ya kazi hiyo, haiwezi kufanyika vizuri. Kwa sababu kila mtu anajua atatoa lawama kwa wengine na hatawajibika moja kwa moja. Lakini mtu mmoja anapowajibika moja kwa moja, atahakikisha wengine wanafanya kazi hiyo vizuri.

Hali hii pia imekuwa inaathiri sana biashara ambazo tunazifanya. Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa lengo la kuuza zaidi, kwa wateja wengi zaidi ili kupata faida kubwa zaidi. Kinachotokea ni biashara inakuwa inalenga kila aina ya mteja na hapo inageuka kuwa haina mteja. Kama biashara ni ya wote, inakuwa haina mteja wa uhakika.

Unafanya biashara yako, mteja anakuja kuulizia kitu ambacho huuzi, unaona ni fursa, unakiweka. Mwingine tena anakuja kuulizia kitu kingine ambacho huuzi, unakiweka. Mwisho unaishia kuwa na biashara ambayo hakuna anayeelewa unafanya nini na hivyo hakuna anayekuja kwako.

Unapokuwa kwenye biashara, lazima uchague kabisa ni aina gani ya wateja unawalenga, kwa kuwa na suluhisho la changamoto au mahitaji yao na kuwalenga hao. Kwa njia hiyo unakuwa unawalenga wateja wa aina fulani na hivyo kuwa na mbinu sahihi za kuwafikia na kubobea kwenye kuwahudumia. Wao wenyewe wanawaambia wengine wenye mahitaji kama yao kuja kwako, kwa sababu unajulikana kutoa huduma fulani inayolenga watu wa aina fulani.

Kumlenga kila mtu inaweza kukuletea faida nzuri kwa muda mfupi, lakini inakuweka kwenye wakati mgumu kukua na kuwafikia walio sahihi. Kuwalenga wachache itakuwa vigumu mwanzoni, itakubidi uzikatae baadhi ya faida, lakini baadaye utakuwa umejenga msingi utakaokusaidia mno, maana kila mtu atajua unafanya nini na hivyo kuwaleta watu sahihi kwako.

Kwa kila kazi unayofanya au kutoa kwa wengine, jiulize nani anayewajibika, kama hakuna mmoja anayewajibika, jua hakuna kazi nzuri itakayokamilika hapo. Na kwa kila biashara unayoifanya, jiulize unalenga mteja wa aina gani, kama unajiambia mteja wako ni kila mtu, jua hapo huna mteja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha