Sumaku huwa ina tabia ya kunasa, lakini huwa hainasi kila kitu.

Sumaku haiwezi kunasa pamba, wala plastiki. Ila sumaku inapokutana na chuma, inakinasa kweli kweli.

Kuna kitu kikubwa cha kujifunza kutoka kwenye sumaku, kuhusu kuchagua watu wa kuambatana nao na kuachana na wengine.

Tunaitumia sumaku kwenye vitu ambavyo inavivuta na hatujisumbui nayo kwa vitu isivyovuta.

Hakuna mtu anaweza kuidharau sumaku kwa sababu tu imeshindwa kunasa plastiki au pamba, tunajua hivyo sivyo vitu inavyoweza kunasa.

Sasa kwa nini unafikiri wewe unapaswa kuendana na kila mtu?

Kwa nini unafikiri biashara yako inapaswa kulenga kila mtu, kupendwa na kukubalika na kila mtu?

Kwa nini unafikiri mawazo yako yanapaswa kukubalika na kila mtu?

Hivyo sivyo asili inavyofanya kazi, hata kama ungekuwa na kitu kizuri kiasi gani na kinachoweza kumsaidia kila mtu, bado kuna watu watakikataa.

Hivyo wajibu wako siyo kuhangaika na kila mtu, bali kuhangaika na wale ambao ni sahihi. Wale ambao tayari wameshanasa kwako, na wewe unapaswa kuwanasa kama sumaku, usiwaachilie kwa namna yoyote ile.

Wale wanaokupenda na ambao unataka wakupende, wapende kweli, usikubali kuwapoteza kwa namna yoyote ile. Hawa ni rahisi kwenda nao kuliko wale ambao inabidi uwalazimishe wakupende.

Kwenye biashara wateja ambao wameshakuelewa na kuielewa biashara yako unapaswa kuwanasa kama sumaku, kwa sababu hawa ni rahisi kuendelea kuwauzia kuliko wapya ambao hawaijui biashara yako.

Kila wakati angalia wale ambao tayari unao na kisha jiulize ni kwa namna gani unaweza kuwanasa zaidi kama sumaku. Angalia nini unaweza kufanya na kuwanufaisha zaidi. Angalia changamoto zote walizonazo na kisha angalia kile unachofanya na ona jinsi gani unaweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto zao.

Nasa kama sumaku, chagua wale utakaokwenda nao na usiwaachie, huku ukiendelea kuchagua wengine wapya utakaoweza kwenda nao. Lakini zoezi la kutafuta wapya lisikufanye uwapuuze wale ambayo tayari unao, hao ndiyo wanapaswa kuwa kipaumbele chako cha kwanza.

Sumaku huwa haiachii ilichonasa ili kunasa kitu kipya, hata kama imejaa huwa inakipa kitu ilichokinasa nguvu ya sumaku na kuvuta vitu zaidi. Kuwa kama sumaku, nasa watu sahihi na watumie hao kunasa wengine sahihi pia.

Kupe pia huwa ana nasa, lakini hatujifunzi kwa kupe, kwa sababu ana nasa kunyonya. Tunajifunza kwenye sumaku kwa sababu ina nasa kutoa nguvu zaidi. Hivyo nasa kama sumaku, siyo kwa kunyonya, bali kwa kutoa nguvu zaidi, na hilo litapelekea wewe kunufaika zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha