Kila maamuzi unayofanya, yanapunguza sehemu ya nguvu ya utashi wako wa kiakili.
Kadiri unavyofanya maamuzi mengi kwenye siku yako, ndivyo unavyochoka kiakili na kushindwa kufanya maamuzi bora.
Na siyo lazima maamuzi yawe makubwa ndiyo yakuchoshe, chochote unachofikiria kwa muda kabla ya kuchukua hatua, kinakula nguvu yako ya akili.
Mfano kama umeamka asubuhi na kuanza kujiuliza uvae nguo gani, hilo linapunguza sana nguvu yako ya kiakili. Kama huna jibu la moja kwa moja nguo gani unavaa, kitendo cha kufikiria na kuanza kulinganisha nguo mbalimbali, kinakuchosha kiakili.
Kama tena utafikiria nini unakula asubuhi hiyo, au unaendaje kwenye shughuli zako, hayo ni mambo yanayoendelea kutumia nguvu yako ya kiakili. Sasa fikiria hiyo ni asubuhi, hata kazi zako hazijaanza lakini umeshafanya maamuzi zaidi ya kumi, ambayo yote yanakuchosha. Haishangazi kwa nini watu wengi wanakuwa wamechoka sana kwenye kazi zao.
Wale wanaojua dhana hii ya kuchoka kwa kufanya maamuzi, huwa wanapunguza sana maamuzi wanayoyafanya, hasa mwanzo wa siku. Huwa wanaamka kwenye muda ule ule kila siku bila ya kujiuliza kama waamke au la, wanavaa nguo ya aina moja au wanaandaliwa nguo ya kuvaa hivyo hawahitaji kufikiria hilo. Kadhalika kwenye kifungua kinywa, wana ambacho wanatumia kila siku au wanaandaliwa kabisa.
Kadiri mtu anavyopunguza maamuzi anayofanya, ndivyo anavyokuwa na nguvu kubwa kiakili na kuitumia kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.
Chunga sana nguvu zako za kiakili, epuka kusumbuka na maamuzi yasiyo na tija yoyote kwako, maeneo mengi ya maisha yako tengeneza mazoea (routine) ambayo utakuwa unaifuata kila siku ili kuepuka kupoteza nguvu kwenye kufikiri kila mara na kufanya maamuzi, hasa kwa mambo madogo madogo.
Tengeneza mwongozo wa siku yako ambao utakuwa unaufuata, unaamka saa ngapi, ukiamia unafanya nini, shughuli zako unafanyaje na mengine muhimu kwenye siku yako. Yale yasiyo ya msingi yasichukue nguvu na muda wako wa mapema.
Nguvu na muda ni rasilimali muhimu lakini zenye ukomo, usipozilinda na kuzitumia kwa kipaumbele kikubwa, utashangaa siku zinaenda na hakuna hatua umepiga kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,