Chochote unachofanya kwenye maisha kwa mategemeo ya kupata kitu fulani, ukiweka juhudi utapata kile unachotaka kufanya. Lakini ukishakipata, huo ndiyo unakuwa mwisho wako, na wakati mwingine kupata ulichokuwa unatafuta kunaweza kuwa sumu na kikwazo kwako kupiga hatua zaidi.
Wale wanaofanikiwa zaidi, wale wanaofanya makubwa kwenye maisha yao, ni wale wanaofanya kitu kwa sababu wanapenda kukifanya na siyo kwa sababu kuna kitu wanategemea kupata.
Unaweza kuona kuna mtego hapo, ukifanya kitu kwa sababu unataka kufanikiwa, hufanikiwi, lakini ukifanya kwa sababu unapenda, unafanikiwa sana.
Hata kwenye fedha, ukifanya kitu kwa sababu unataka kupata fedha nyingi, huzipati, lakini unapofanya kile unachopenda, unapata fedha nyingi kuliko ulivyotegemea.
Somo hapa siyo uache kile unachofanya kupata fedha, kwa sababu fedha unazihitaji na unahitaji mahali pa kuanzia.
Somo kuu hapa ni kuangalia maisha yako kwa miaka mingi ijayo, kuangalia ndoto kubwa ulizonazo na kisha kujua nini hasa unapenda kufanya. Nini uko tayari kufanya muda wote hata kama hakuna anayekuangalia. Kisha kuanza kufanya kitu hicho mapema na kukifanya bila ya kuacha. Kadiri muda unavyokwenda na jinsi unavyoendelea kufanya, unayafikia mafanikio makubwa.
Lakini hata unapofanya, hukazani sana na mafanikio, bali unakazana na kufanya kwa sababu hayo ndiyo maisha yako, na hujioni ukifanya kitu kingine isipokuwa hicho.
Kama bado hujajua kile unachopenda kufanya, jukumu lako la kwanza ni kujua kitu hicho. Changamoto ni kwamba hakuna njia ya mkato ya kujua hilo, hakuna mwingine anayeweza kukuambia, ni kitu cha kukifikia wewe mwenyewe. Hivyo fanya zoezi la kujitambua binafsi, kujua nini unapendelea sana kufanya na weka mkakati wa kuanza kufanya na kufanya kila siku au mara kwa mara.
Kama umeshajua unachopenda kufanya ila hujaanza kukifanya, jipange kuanza kukifanya sasa.
Kama umeshajua unachopenda kufanya na umeanza kukifanya, lakini hujaweza kuingiza kipato kupitia kitu hicho, waangalie wale wanaonufaika sana na unachofanya, wanaokusifia kwa unachofanya, wanaokushukuru jinsi unachofanya kinawasaidia, kisha angalia wana changamoto zipi ambazo unaweza kuwasaidia kuzitatua na wakakulipa. Anza hata na mmoja, kisha nenda wachache na endelea kukua hivyo. Wakati ukijenga hilo, hakikisha kuna kitu kingine unachofanya cha kukuingizia kipato cha kuyaendesha maisha yako, na hata kama siyo unachopenda hasa, kwa wakati huu unapokuwa unakifanya, kipende.
Kama umeshajua unachopenda kufanya na tayari watu wanakulipa kwa kukifanya, hongera. Lakini jua hujafika mwisho, kila siku lazima ukazane kuwa bora, lazima uende hatua ya ziada na kutoa thamani kubwa zaidi kwa wengine. Siyo kwa sababu kuna matokeo unategemea, ila kwa sababu unapenda kweli kufanya kitu hicho.
Fanya kile unachopenda kufanya kutoka ndani ya moyo wako, na siyo kile unachofanya ili kupata matokeo fulani, kisha kifanye kwa moyo wako kweli, jisukume, kifanye kwa ubora wa hali ya juu na utapata matokeo makubwa na mazuri ambayo hujawahi kuyafikiria wala kuyategemea.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,