Watoto wadogo na wanyama huwa ni nadra sana kupatwa na msongo wa mawazo.

Hiyo ni kwa sababu wanaishi kwenye wakati uliopo, wanakabiliana na kilicho mbele yao.

Ni vigumu kumkuta kuku akiwa na msongo kwamba kesho yake utakuwaje au kuhusu jana iliyopita au akihofia kuhusu yale yanayoendelea kwenye dunia. Kuku anakabiliana na kile kilicho mbele yake, kupata chakula, kujilinda yeye pamoja na vifaranga wake.

Kadhalika kwa mtoto, hata anapokuwa amekosea na akaadhibiwa, baada ya muda anasahau kabisa adhabu ile na kuendelea na mambo mengine. Huwezi kumkuta siku nyingi baada ya adhabu akiendelea kuikumbuka na kuumizwa nayo, hata kama haikuwa sahihi.

Japo sisi watu wazima tuna utofauti mkubwa na watoto au wanyama, kwa sababu tuna utashi, bado tuna mengi ya kujifunza kutoka kwao. Na moja kubwa ni kuweka fikra zako pale ulipo sasa, kwenye kile unachofanya sasa. Usiruhusu fikra zako zihangaike maeneo mengine, huko ni kukaribisha hofu na msongo wa mawazo.

Kama utajiweka kweli kwenye kile kilicho mbele yako, hata kama ni kidogo kiasi gani, kitakuwa kinga kubwa kwako usipate msongo au kusumbuliwa na hofu.

Vitu vingi vinavyokupa hofu na msongo ni vitu ambavyo huwezi kuviathiri au kuvibadili kwa wakati unasumbuka navyo, na hapo vinakuondoa kwenye kile unachofanya. Hilo linapelekea usifanye vizuri kile unachofanya sasa na baadaye kinakuja kuwa chanzo cha msongo tena.

Kata huo mnyororo, chagua kufanya kitu kwa ukamilifu wake, kwa kuweka juhudi zako zote kwenye hicho unachofanya na fikra zako kuwa hapo. Na chochote kinachokuja kwenye mawazo yako ambacho ni tofauti, kiandike mahali na uje ukifanyie kazi baadaye, lakini kwa sasa, usiondoe fikra na juhudi zako kwenye kile unachofanya.

Hatua ya kwanza ya kuwa na utulivu na furaha kwenye maisha ni kuwa pale ulipo bila ya kuruhusu fikra zako kuzurura sehemu nyingine yoyote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha