Kuna kauli moja fupi ila yenye maana kubwa sana, kauli hiyo inasema muda huwa ni tiba ya kila kitu. Chochote kinachoshindikana, kipe muda.

Muda una nguvu kubwa, hasa unapokuwepo wa kutosha. Lakini wengi huwa hawaweki muda wa kutosha kwenye kitu chochote wanachofanya.

Matokeo yake wanalazimika kutumia nguvu kubwa ili kulazimisha matokeo. Kwa kutumia nguvu wanaweza kupata matokeo wanayotaka, lakini huwa nguvu hizo zinazalisha madhara baadaye.

Chukua mfano wa kuwafanya watu wakubaliane na kitu ambacho hawakubaliani nacho. Unaweza kutumia mbinu za ushawishi, jambo ambalo lina hitaji muda mpaka mtu aelewe kweli. Au unaweza kutumia nguvu na mabavu, kwa kumwambia mtu lazima ufanye hivi, kama una mamlaka juu yake atalazimika kufanya, kwa sababu hana namna. Lakini mtu huyo hatakuwa amekubali kitu hicho kutoka ndani yake, hivyo hatakifanya vizuri.

Kwa jambo lolote unalotaka kufanya, jipe muda wa kutosha, usikimbilie njia ya mkato ya kutumia nguvu na mabavu, unaweza kukamilisha, lakini haitakuwa kwa ubora.

Na hili unapaswa kuwa nalo makini pale unapokuwa na mamlaka fulani. Hata kama ni mzazi, unaweza kuona una nguvu ya kuwalazimisha watoto wako kufanya unavyotaka wewe, lakini kutumia nguvu hiyo kutaathiri mahusiano yako na wao. Ukitumia ushawishi, utakusaidia kuwafanya watekeleze huku pia ukiboresha mahusiano yako na wao.

Kadhalika kwenye kazi, chukua mfano una jukumu la kukamilisha siku 30 zijazo, kwa siku za mwanzo hutakuwa na msukumo wa kufanya jukumu hilo. Siku zinaenda, huchukui hatua kubwa. Lakini inapobaki siku moja jukumu kuisha unafanya kazi usiku na mchana kulikamilisha. Ulikuwa na muda hukufanya, muda umeisha unalazimika kutumia nguvu za ziada. Japokuwa utakamilisha jukumu, lakini haitakuwa kwa ubora na wewe utabaki ukiwa umechoka sana.

Mara zote fikiria sana kuhusu muda na nguvu, na hilo litakufanya uuthamini muda ili usilazimike kutumia nguvu ambazo baadaye zinakuwa na madhara.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha