“Grow spiritually and help others to do so; it is the meaning of life.” – Leo Tolstoy

Maana ya maisha yetu na jukumu kubwa kabisa tulilonalo hapa duniani ni kukua kiroho.
Changamoto nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha na kutuyumbisha, ni kwa sababu ya uchanga wa kiroho.
Unapokua kiroho, unaweza kukabiliana na changamoto yoyote ile huku ukiwa na utulivu mkubwa ndani yako.

Ukuaji wa kiroho hautaziondoa kabisa changamoto, bali utakuwezesha kukabiliana na kila aina ya changamoto bila ya kuhofia.
Ukuaji wa kiroho hautayafanya maisha kuwa rahisi, bali utakufanya wewe kuwa ngumu na kuweza kupambana na kila kinachokujia kwenye maisha.

Ukuaji wa kiroho ndiyo kipimo cha imani ambayo mtu anayo.
Haijalishi mtu unaamini nini, usahihi na manufaa ya kile unachoamini ni jinsi kinavyokusaidia kiroho na kuweza kuyaishi maisha yako kwa utulivu.

Ukuaji wa kiroho siyo kitu cha kuiga kwa wengine, kuonesha wengine au kushindana.
Bali ni maisha unayokuwa umeyachagua baada ya kujitambua wewe mwenyewe na kujua kile hasa unachotaka.

Dini zilipaswa kuwasaidia watu kukua kiroho, lakini nyingi hazifanyi hivyo. Zinakazana na vitisho na hofu ili ziweze kuwatawala waumini wake.
Falsafa zilipaswa kuwasaidia watu kukua kiroho lakini wengi hawajifunzi falsafa ili kuiishi, badala yake wanajifunza pale wanapolazimishwa kufanya hivyo, labda shuleni, au wanapotaka kitu cha kubishana.

Hivyo jukumu la ukuaji wa kiroho linabaki kwenye mikono yako mwenyewe,
Usitegemee mtu aje kukusaidia kwenye hili.
Jijengee mfumo wa imani ambao ni bora na sahihi kwako.
Lijue kusudi la maisha yako hapa duniani na pambana kuliishi kusudi lako.
Kila wakati pambana kukua zaidi kiroho na kuwawezesha wengine kukua kiroho pia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kujifunza na siyo kuiga, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/12/23/2184

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.