Ukila chakula, kinameng’enywa tumboni, kisha kufyonzwa mwilini na kwenda kuwa sehemu ya mwili wako. Hivyo kila unachokula, kinaenda kuwa sehemu ya wewe.
Kadhalika kwenye yale tunayofanya, huwa yanakuwa sehemu yako, yanakuwa wewe.
Kitu chochote unachofanya kwa kujirudia rudia, kinaenda kuwa tabia ambayo inakuwa sehemu yako.
Hivyo chochote kile unachofanya, humfanyii mtu mwingine yeyote, bali unajifanyia wewe.
Kama kuna mtu unamchukia kwa sababu alikufanyia kitu ambacho siyo sahihi, humchukii yeye, bali unajichukia wewe mwenyewe. Chuki unayoijenga inabaki kuwa sehemu yako, unakuwa mtu wa chuki, utajichukia mwenyewe na kuwachukia wengine ambao hawajakukosea chochote.
Kama umepewa kazi na mtu ufanye, ila anakulipa kidogo na wewe ukaamua kuifanya hovyo kwa sababu mtu huyo hakujali, kufanya kwako kazi hovyo hakumuathiri sana yule unayemfanyia kama kunavyokuathiri wewe mwenyewe. Kila kazi unayoifanya inakuwa sehemu yako, inakuwa wewe.
Umewahi kujiuliza kwa nini watu wanakuwa kwenye ajira ambazo hawazipendi, wanazoifanya basi tu ili wapate mtaji wa kwenda kuanza biashara, wanaupata na kwenda kuanza biashara, ila hazidumu muda zinakufa? Ni kwa sababu walipokuwa wanafanya kazi walikuwa wanafanya hovyo, ikajijenga na kuwa tabia, hivyo hata wanapoenda kuanzisha biashara zao, wanaziendesha kwa tabia ile waliyojijengea kwenye ajira na ndiyo maana zinashindwa.
Kwa kujua hili, kuwa makini sana na chochote unachofanya, kwa sababu humfanyii mtu mwingine yeyote, bali unajifanyia wewe mwenyewe. Kinabaki kuwa sehemu yako, inakuwa tabia iliyojijenga kwako na itakuwa na madhara baadaye.
Chochote unachofanya, kifanye kweli kutoka ndani ya moyo wako, ukikifanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa au achana nacho kama huwezi kukifanya hivyo. Ni bora usifanye kabisa kuliko kufanya na kujijengea tabia itakayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako ya baadaye.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,