Mafanikio yana maana tofauti kwa watu tofauti, lakini watu waliofanikiwa wanafanana kwa mengi, hata kama siyo kwa fedha na mali walizonazo.

Wale waliofanikiwa kuna vitu wanakuwa wameshinda, ambavyo vinayafanya maisha yao kuwa tulivu na hivyo kuweza kupeleka umakini mkubwa kwenye kile wanachofanya badala ya kuhangaika na yasiyo sahihi.

Kuna maeneo manne muhimu unayopaswa kushinda ili kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Eneo la kwanza ni kwenye kazi au biashara unayochagua kufanya, inapaswa kuwa sahihi kwako lakini pia yenye fursa ya ukuaji zaidi, kwa kuwahudumia wengi na kuweza kutengeneza kipato kizuri na cha uhakika. Epuka vitu vya msimu na visivyo sahihi.

Eneo la pili ni uwekezaji, unapaswa kuwa na uwekezaji ambao unaongezeka thamani na kuzalisha faida. Uwekezaji ndiyo njia ya kujihakikishia unakuwa na kipato cha baadaye hata kama huwezi kufanya tena kazi.

Eneo la tatu ni mwenza unayechagua kuwa naye kwenye maisha. Mwenza wako ana mchango sana kwenye utulivu na mafanikio ya maisha yako, unapaswa kuchagua ambaye mnaelewana na kuendana.

Eneo la nne ni kujikubali na kujithamini wewe mwenyewe. Hayo mengine yote hayatakuwa na maana kama wewe mwenyewe hujikubali na kujithamini. Hili ndiyo linakupa wewe nguvu ya kuchagua kufanya kazi au biashara sahihi, kuwa na mwenza sahihi na pia kufanya uwekezaji.

Ukishinda maeneo haya manne, una uhakika wa kuwa na maisha bora, tulivu na yenye mafanikio makubwa. Yafanyie kazi maeneo haya kila siku. Kwa kuweka thamani zaidi kwenye kile unachofanya, kuwa na uwekezaji endelevu, kuboresha mahusiano yako na mwenza wako huku ukijikubali na kujithamini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha