Leo nasema na wale wanaotoa huduma mbalimbali kutokana na ujuzi, maarifa na uzoefu walionao.

Wengi mmekuwa mnafanya hivyo bure kabisa, bila ya kutoza gharama zozote kwa wale wanaopokea huduma mnazotoa.

Inaweza kuwa ni uandishi ambapo unaandika makala ambazo watu wanasoma bure mitandaoni.

Pia inaweza kuwa ni ushauri ambao watu wanakuomba kulingana na eneo ulilobobea na wewe unawapa ushauri huo bure bila kuwatoza chochote.

Wengi watakuwa wanakusifia kwa moyo wako wa kujitoa, kwa jinsi unavyowajali wengine na kuwapa kile ulichonacho, tena bila ya tamaa ya kutaka kulipwa chochote.

Huenda umefanya hivyo kwa muda na umekuwa unajaribu sana kulipwa kwa unachofanya. Unajaribu kuwaambia watu wakulipe kwa huduma unazowapa. Lakini wengi wanakuwa hawapo tayari kufanya hivyo, wengine wanaenda mbali zaidi na kukuhukumu kwamba umekuwa na tamaa, unajali kulipwa zaidi kuliko kuwasaidia wengine.

Rafiki yangu mpendwa, kama unaambiwa hivyo au umewahi kufikiria hivyo na kuona ni sahihi kuendelea kutoa huduma zako bure basi unajidanganya.

Kwa chochote unachofanya, ambacho kina thamani kwa wengine, basi unapaswa kulipwa kwa thamani unayozalisha.

Kama hulipwi basi kutakuwa na tatizo moja kati ya haya mawili;

Moja ni huduma unayoitoa haina thamani kwa wale wanaoipokea, kiasi kwamba hawaumii hata kama wataikosa. Kama kitu kinapatikana kwa urahisi hakuna anayekuwa tayari kukilipia.

Mbili ni watu unaowalenga siyo sahihi, ni watu ambao hawathamini kile unachofanya na hivyo hawaoni umuhimu wa kulipia.

Ukiweza kutatua hayo mawili, basi utaweza kulipwa kwa kile unachofanya.

Mwaka 2021 ni mwaka wa wewe kulipwa kwa kila unachofanya, usikubali tena kuendelea kudanganywa kwamba unafanya kwa kusaidia.

Jua watu hao hao wanaokuambia huduma yako inapaswa kuwa msaada, kila siku wanawasiliana na wengine, wanaingia mitandaoni kufuatilia mambo haya yasiyo muhimu. Lakini hawayaambii makampuni ya simu yawape vocha za bure kwa sababu wanapaswa kusaidia, wanatoa fedha na kununua vocha.

Jua hao wanaokuambia unapaswa kutoa huduma yako bure kama sadaka na msaada, wakienda kwenye nyumba za ibada wanatoa sadaka ambayo ni pesa. Hawawaambii viongozi wao wa dini kwamba wanapaswa kuwahudumia bure, wanatoa sadaka vizuri tu.

Sasa kwa nini watu hao wawe tayari kumlipa kila mtu isipokuwa wewe?

2021 ni mwaka wa kubadili hilo, na kuhakikisha unalipwa kwa kile unachofanya. Kwa sababu unawekeza muda na nguvu kwenye kitu hicho, muda ambao huwezi kuutumia kwenye vitu vingine.

Hatua za kuchukua.

Kama unafundisha, kushauri au kuongoza wengine kupitia ujuzi, maarifa na uzoefu ulionao, basi tengeneza mfumo wa wao kukulipa au kuchangia huduma wanayopata kwako.

Njia ya kufanya hivyo ni kuwa na mifumo miwili ya kutoa huduma zako.

Mfumo wa kwanza ni wa bure kabisa, hapa unatoa mafunzo na ushauri ambao ni wa jumla na wenye miongozo sahihi ya mtu kufuata ili kutatua changamoto au kupiga hatua.

Mfumo wa pili ni wa kulipia, ambapo yule aliyepata mafunzo ya bure na kufanyia kazi kisha akapata matokeo mazuri, akitaka kupata zaidi kutoka kwako, basi analipia gharama na unampa zaidi.

Kwenye mfumo huo wa pili unakuwa na ushauri wa moja kwa moja na mafunzo ya ngazi ya juu zaidi, yanayomwezesha mtu kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yake.

Ukishakuwa na mifumo hii miwili, chagua watu ambao unawalenga, ambapo wana uhitaji kweli na wanathamini kile unachofanya, ambao watafanyia kazi na kupata matokeo ya tofauti.

Baada ya kujua watu gani unaowalenga, weka thamani kubwa kwenye mifumo yote miwili. Kwenye mfumo wa bure weka thamani kubwa kiasi kwamba mtu anaelewa na kuweza kuchukua hatua zinazoleta mabadiliko kwenye maisha yake. Kwenye mfumo wa pili, toa mafunzo au ushauri ambao mtu hawezi kuupata sehemu nyingine yeyote.

Ndiyo unataka kulipwa, lakini jua kabisa kwamba kutoa fedha huwa kunauma, ili mtu aitoe fedha yake aliyoitafuta kwa jasho, lazima kuwe na kitu chenye thamani anachokipata. Hivyo unapaswa kutoa mafunzo na ushauri ambao una manufaa kwa mtu, lakini pia hawezi kuupata sehemu nyingine ile isipokuwa kwako. Kwa namna hiyo, unapomwambia mtu alipie, atafanya hivyo kwa sababu ni kitu chenye manufaa na hakipatikani pengine.

Toa thamani kubwa na walenge walio sahihi ndiyo miongozo mikubwa kwako kulipwa kupitia utoaji wa huduma binafsi kwa mwaka 2021, ufanyie kazi kila siku.

Njia nyingine za kulipwa kupitia huduma zako binafsi 2021 ni hizi;

1. Andika vitabu vinavyojibu changamoto ambazo watu wanakutafuta sana uwasaidie. Mtu anapokutafuta, mwelekeze kitabu ulichoandika kinachojibu changamoto yake ili akinunue.

2. Kuandaa kozi mbalimbali ambazo watu wanaweza kujifunza kwa njia ya mtandao au nyinginezo.

3. Kutoa ushauri wa moja kwa moja kwa gharama ambayo mtu anailipa kabla ya kupata ushauri.

4. Kuwaweka watu kwenye kundi na kisha kuwapa mwongozo kama kikundi.

5. Kufanya kazi na mtu mmoja mmoja kwa karibu ili aweze kupiga hatua kwenye kile anachotaka.

Kwa njia yoyote utakayotumia, hakikisha unatoa thamani kubwa na yenye matumizi kwa unaowalenga, lakini pia hakikisha hawawezi kupata thamani hiyo sehemu nyingine yoyote isipokuwa kwako.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania