Sisi binadamu huwa tunachekesha na kuhuzunisha kwa wakati mmoja.

Mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu kufanya huwa hatuyafanyi, bali yaliyo nje ya uwezo wetu ndiyo tunahangaika nayo.

Mambo yaliyo muhimu na yenye manufaa kwetu huwa hatuhangaiki nayo, ila yale yasiyo muhimu na yasiyo na manufaa kwetu ndiyo yanatuhangaisha.

Huwa tunakazana kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa, halafu tunatumia muda mwingi kulalamika ni jinsi gani maisha ni magumu.

Ni wakati sasa wa kuokoa na kutunza nguvu na muda wako, kwa kuvipelekea kwenye mambo machache muhimu, yaliyo ndani ya uwezo wako, muhimu na yenye manufaa kwako.

Tukianza na iliyo ndoto ya wengi, ya kutaka kuibadili dunia, hili ni jambo ambalo hupaswi kuhangaika nalo. Dunia ni kubwa na inajiendesha yenyewe, hata kama wewe usingekuwepo ingeendelea kwenda.

Lakini kuna kitu unaweza kufanya na kikachangia dunia kubadilika, kwa kuanzia hapo ulipo sasa. Anza kwa kubadilika wewe mwenyewe, kisha wasaidie wanaokuzunguka kubadilika na kwa njia hiyo utaweza kuleta matokeo ya tofauti kwenye dunia.

Siyo unahangaika na kuibadili dunia, wakati familia yako yenyewe imekushinda. Siyo unakazana kuwabadili wengine, wakati wewe mwenyewe umeshindwa kubadilika.

Ukitupa jiwe baharini, huwa linazalisha mawimbi ambayo yanasambaa kwenye eneo kubwa. Hivyo pia ndivyo mabadiliko yanayoanzia ndani yako na kwa wale wa karibu yanavyosambaa kuifikia dunia nzima.

Anza wewe kuishi kwa misingi sahihi, utapata matokeo ambayo ni ya tofauti, wale wa karibu kwako watataka kujua nini kinakupa matokeo ya tofauti, waoneshe. Na wao wakitaka watafanya kama wewe, na kuzalisha matokeo ya tofauti kitu kitakachowavutia wengi zaidi.

Kidogo kidogo mabadiliko uliyoanzisha yanasambaa na kuwafikia wengi, bila ya wewe kuhangaika na kuumia.

Unapoanza na lengo la kutaka kuibadili dunia, unajiandaa kuangushwa na kukatishwa tamaa. Maana kila unachojaribu kufanya kwa ajili ya wengine, kitapingwa, kubezwa na kudharauliwa.  Lakini unapoamua kubadilika wewe mwenyewe, unapoamua kuwa tofauti, watu watakupinga, lakini hawawezi kukuangusha kama umeamua kusimama kweli. Na uzuri ni pale utakapokuwa umefanikiwa, hawatakuwa na budi bali kukusikiliza.

Muda wako ni mfupi, nguvu zako zina ukomo, usizitawanye hovyo kuhangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wako au yasiyo na manufaa. Wekeza rasilimali hizo muhimu kwa usahihi na utapata matokeo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha