Siku utakayokuwa unavuta pumzi yako ya mwisho hapa duniani, kuna mambo utajivunia kwa kuyafanya na kuna mambo utajutia kuyafanya.
Hiki ni kitu ambacho wengi huwa hawakifikirii mapema, lakini wanapofika ukingo wa maisha yao ndiyo wanapata nafasi ya kuyatafakari maisha yao, huku wakiwa hawana cha kubadili.
Lengo lako kwenye maisha ni kuishi kwa namna ambayo siku unavuta pumzi yako ya mwisho, utakuwa na mengi ya kujivunia kufanya huku ukiwa na machache ya kujutia kufanya.
Hivyo chochote unachofanya sasa, jiulize kitakupa matokeo gani na siku ya kuvuta pumzi yako kama utajivunia au utajutia.
Mambo yote mazuri unayoyafanya, yenye mchango kwako na kwa wengine, utajivunia nayo mpaka siku ya mwisho.
Lakini mambo ya hovyo unayohangaika nayo, utayajutia sana.
Siku yako ya mwisho hutajivunia kuwepo kwenye mitandao ya kijamii kila siku, kubishana na watu mambo mbalimbali au kuahirisha yale uliyokuwa unapanga kufanya.
Lakini utajivunia kile ulichoanzisha, iwe ni mradi au biashara ambayo imekuwa na mchango mzuri kwa wengine. Utajivunia ushuhuda ambao wengine wamekupa wa jinsi umebadili na kuboresha maisha yao.
Kinachofanya wengi tuhangaike na mambo tunayokuja kuyajutia baadaye ni kuona tuna muda mwingi. Mfano kwa nini unaahirisha kuanza unachopanga? Ni kwa sababu unajipa uhakika kesho ipo. Vipi kama leo utaambiwa huna kesho, leo ndiyo mwisho wako, kwa hakika hutaahirisha chochote.
Hivyo kujisukuma kufanya yaliyo sahihi kwako, jione huna muda. Usijidanganye kwamba kesho ipo, chukulia leo ndiyo siku yako ya mwisho na hivyo fanya kile ambacho hutajutia.
Uhakika tulionao ni kwamba, kuna siku itakuwa ya mwisho kwetu, lakini kwa bahati mbaya hatuijui siku hiyo ni lini. Kwa nini usianze sasa, usichukulie kila siku unayoipata ni ya mwisho na kuiishi kwa ukamilifu wake? Utafanya yaliyo bora, utakayojivunia nayo kwa siku zote za maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,