Kuna majukumu ambayo unapenda kuyafanya, ambayo upo tayari kuyafanya kwa muda mrefu iwezekanavyo, haya siyo shinda kwako kama ni majukumu muhimu.

Ila kuna majukumu ambayo hupendi kuyafanya kabisa, kila ukifikiria kuyafanya unajikuta ukiahirisha na kupanga kufanya mambo mengine.

Tatizo la majukumu haya yanakuwa ni muhimu sana, kiasi kwamba usipoyafanya basi yanakuwa na madhara makubwa kwako baadaye.

Wengi hujikuta wakiahirisha majukumu haya mpaka tarehe ya mwisho kuyafanya inafika na kusumbuka zaidi. Au wanayaahirisha mpaka inafika hatua yanakuwa mzigo mzito na kikwazo kikubwa kwa maisha ya mtu.

Ipo njia nzuri ya kuhakikisha aina hiyo ya majukumu unayatekeleza kabla ya muda kuisha.

Njia hiyo ni kutenga muda mfupi wa kufanya jukumu husika. Anza na muda mfupi kabisa, mfano dakika 15. Tenga dakika 15 za kufanya jukumu hilo, kisha jiambe utalifanya kwa dakika 15 tu.

Hakuna anayeshindwa kufanya chochote kwa dakika 15, hivyo acha mengine kwa dakika hizo 15 na anza kufanya jukumu hilo. Weka kabisa kipima muda kujua pale dakika hizo 15 zinapoisha.

Dakika 15 ulizopanga kufanya kitu zinapoisha, jiulize kama unataka kuendelea kufanya kitu hicho, kama ndiyo basi endelea kufanya. Kama hutaki kuendelea acha na fanya kingine unachotaka. Panga tena dakika 15 za kufanya kitu hicho baadaye.

Uzuri wa njia hii ni kwamba ukishatenga muda mfupi wa kufanya kitu na kuanza kukifanya, utajikuta ukitaka kuendelea kukifanya kwa muda zaidi. Kinachokuwa kinakukwamisha ni kuanza, kwa vile unaliona jukumu gumu na kinalohitaji muda mrefu, unajiambia sasa huna muda na hivyo kuahirisha.

Unapojipangia muda mfupi, kigezo cha huna muda kinafutika, unaanza kufanya na ukishaanza unagundua jukumu siyo gumu kama ulivyokuwa unalichukulia na hivyo kujikuta unaendelea kulifanya kwa muda mrefu.

Hata kwenye kusoma vitabu, unaweza kukiangalia kitabu na kukiona ni kikubwa na kigumu hivyo huwezi kukisoma. Lakini jipe dakika 10 za kusoma kwa wakati mmoja na utaikuta ukikisoma kwa muda mrefu na hata kukikamilisha.

Chochote unachosua sua kuanza, chochote unachoahirisha kwa kuona huna muda, tenga muda mfupi wa kukifanya na kisha anza. Muda huo ukiisha jitathmini kama unataka kuendelea endelea, kama hutaki acha. Kwa njia hii utaweza kufanya mengi na makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha