Miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, mwanafalsafa Seneca aliandika; tatizo la muda siyo kwamba tuna uhaba nao, ila tuna muda mwingi mpaka tunaamua kuupoteza.
Aliendelea kueleza kupitia insha yake aliyoiita On The Shortness Of Life; muibie mtu pesa au mali yake na atapambana na wewe mpaka umrudishie ulichomuibia, lakini muibie mtu muda wake na hatajisumbua kuulinda, atakuacha uibe utakavyo.
Akasisitiza zaidi kwa kusema; huwa tunakuwa na uhaba na vitu tunavyoweza kuvipata tena, lakini tunatawanya hovyo vile ambavyo vikishapotea havirudi tena.

Rafiki yangu, maneno hayo yaliandikwa zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, wakati ambao hapakuwa na tv, hapakuwa na kompyuta wala instagram. Lakini angalia maisha tunayoyaishi sasa, unaweza kufikiri Seneca yuko na sisi sasa, akituangalia tunavyohama kutoka wasap, kwenda faebook, kisha kwenda instagram kabla ya kumalizia kwenye tv. Halafu hapo hapo tunalalamika hatuna muda wa kusoma vitabu, hatuna muda wa kuanzisha au kukuza biashara ili kuongeza kipato chetu.
Seneca aliandika miaka mingi iliyopita, lakini mpaka leo tunarudia makosa yale yale, tunatapanya muda wetu hovyo, halafu tunalalamika hatuna muda.
Rafiki, leo nataka niwe muwazi kwako, maana nimechoka kusikia watu wakilalamika hawana muda. Na wala sivumbui chochote kipya, nakuonesha tu jinsi Seneca alikuwa sahihi miaka elfu mbili iliyopita.
Ninachotaka kukuambia wazi ni kwamba kama unasema huna muda, wewe ni muongo. Siyo kweli kwamba huna muda, ila unatumia muda wako hovyo. Ndiyo unaianza siku na kuimaliza ukiwa umechoka, hupati hata muda wa kupumzika, lakini unazalisha nini? Ukijitathmini jinsi unavyoziishi siku zako, utaona jinsi sehemu kubwa ya muda wako unaupoteza kwenye mambo yasiyo muhimu.
Hivyo anza kwa kujiambia hili; sehemu kubwa ya muda wangu naupoteza kwa mambo yasiyo sahihi. Wanasema kujua tatizo ni nusu ya kulitatua. Umekuwa unahangaika na muda maisha yako yote kwa sababu hujui tatizo, tatizo siyo muda ni mfupi, tatizo ni unapoteza muda.
Kuthibitisha kwamba kweli unapoteza muda, chukua kalamu na karatasi na fanya zoezi hili.
Gawa karatasi yako kwenye pande mbili.
Upande mmoja andika ndoto na malengo unayotaka kufikia.
Upande wa pili orodhesha mambo yote uliyofanya kwa wiki moja iliyopita. Kila ulichofanya, iwe uliangalia tv, uliingia instagram, ulibishana na mengine, orodhesha.
Kisha chora mstari, kutoka kwenye kile ulichofanya kuelekea kwenye lengo ambalo kimesaidia kufikia. Yaani kwa kila ulichofanya, oanisha na upande wa malengo, kimesaidia kufikia lengo au ndoto gani.
Hapo utajionea wazi ni jinsi gani mambo mengi uliyofanya hayakuwa na mchango wowote kwako kufikia malengo yako, na hivyo ulipoteza huo muda uliyafanya.
Kubali ukatae, unapoteza muda mwingi mno, muda ambao ungeweza kuuokoa na kuutumia vizuri, ungefanya makubwa mno. Ungeshaanzisha na kukuza biashara unayoifikiria kwa muda mrefu sasa. Ungeshaandika kitabu ambacho unajiambia utaandika. Ungekuwa na mahusiano bora na wale wa karibu kwako.
Lakini huna vitu hivyo na huna muda! Ni kichekesho kilichoje?
Hatua za kuchukua.
Leo nakupa hatua kubwa mbili za kuchukua rafiki yangu, ili usilalamike tena kwamba huna muda.
Hatua ya kwanza ni kufanya tathmini niliyokushirikisha hapo juu na kila unapoianza siku yako, orodhesha malengo na ndoto kubwa unazofanyia kazi, kisha orodhesha mambo unayokwenda kufanya kwenye siku hiyo ili ufike kwenye ndoto na malengo hayo. Kisha kwenye siku yako fanya yale tu uliyopanga. Kutokana na tathmini uliyofanya, kuna mambo utakuwa umeona unayafanya mara kwa mara na hayana mchango, jiambie wazi kwamba hutayafanya tena mambo hayo.

Hatua ya pili ni kusoma kitabu nilichoandika, kinachoitwa PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU. Kwenye kitabu hiki nimekuonesha jinsi ya kupata muda zaidi kwenye siku yako na baada ya kupata muda huo nimekushauri jinsi ya kuutumia vizuri ili uweze kubadili maisha yako. Kitabu ni nakala tete na kinapatikana kwenye APP YA SOMA VITABU, kukipata pakua na kuweka app ya soma vitabu kwenye simu yako, fungua hapa; http://bit.ly/somavitabuapp maelezo ya jinsi ya kutumia app na kununua vitabu fungua kiungo kilicho hapo chini.
Rafiki, nihitimishe kwa kukusisitiza tena kwamba muda unao, tena mwingi mno, ila unautapanya hovyo na kuruhusu wengine wauibe na kuuchezea watakavyo. Kama kweli unataka kufanikiwa na kuwa na maisha bora, acha kujidanganya kuhusu muda, chukua hatua mbili nilizokushauri hapa na utaweza kufanya makubwa.
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania