Viumbe hai wengine wote ukiacha binadamu, huwa wanazaliwa wakiwa tayari wana njia ya kuyaendesha maisha yao. Wanakuwa tayari kukabiliana na mazingira yao pale wanapokuwa wamezaliwa na wanayaendesha hivyo maisha yao.

Binadamu ndiye kiumbe hai pekee anayezaliwa akiwa hana maandalizi kamili ya kukabiliana na maisha yake, ndiyo maana anachukua muda mrefu kulelewa na mzazi wake kuliko viumbe wengine.

Namna ya kuendesha maisha, mtu anajifunza kwa namna anavyoishi. Hivyo tangu ukiwa mdogo umekuwa unakusanya maarifa na taarifa mbalimbali ambazo ndiyo umekuwa unazitumia kufanya maamuzi kwenye maisha yako.

Ubaya ni siyo yote unayojifunza unajua kama umejifunza, bali unapofika wakati unaohitaji hali fulani, unajikuta umeshafikia hali hiyo bila hata ya kufikiria sana.

Watu wanapokuwa kwenye msongo, hisia kali au ulevi, kuna vitu huwa wanafanya lakini wakiondoka kwenye hali hizo wanavijutia na kusema waliteleza. Wanasingizia zile hali kama ndiyo chanzo cha wao kufanya waliyofanya.

Hiyo ni njia tu ya kujifariji, lakini msongo, hisia au ulevi haviongezi fikra zozote kwenye akili yako za maamuzi gani ufanye, bali zinazuia fikra na kukupeleka kwenye mazoea.

Yale unayofanya ukiwe kwenye msongo, hisia au ulevi ni mambo ambayo tayari yapo ndani yako, umekuwa unayafikiria kwa muda mrefu, lakini umekuwa huyaweki wazi kwa sababu fikra zako za kawaida zinajua siyo mambo sahihi.

Sasa inapotokea fikra za kawaida zimefungwa na vitu vinavyofunga fikra hizi ni msongo, hisia na ulevi, yale uliyokuwa unayaficha hayana pa kujificha tena, hivyo yanatoka bila kizuizi.

Kama umekuwa na hasira kali na kusema au ukafanya kitu ambacho baadaye unakijutia, cha kulaumu siyo hasira, hasira hazijaongeza kitu kipya kwako, bali zimekufanya usiweze kufikiri kwa usahihi na hivyo kurudi kwenye mazoea yako.

Hivyo cha kufanya ni kubadili mazoea yako, kubadili namna unavyofikiri ndani yako kwa muda mrefu, kile ambacho watu hawakioni.

Mfano kama muda mwingi umekuwa unafikiri kwa upande wa chuki, matusi na kupiga wengine, utakapokuwa katika hali ambayo huwezi kufikiri kwa usahihi, utaishia kutukana au kupigana.

Lakini kama muda mwingi unafikiri kuhusu upendo, kuwajali wengine na kuwachukulia kama walivyo, unapokuwa kwenye hali inayokuzuia usifikiri, utaikabili vizuri. Hata kama ni mtu amekutukana na ukapatwa hasira, utajikuta unamuonea huruma badala ya wewe kumrudishia matusi na jambo dogo likawa kubwa.

Kila unapojikuta umesema au kufanya jambo ambalo unajutia, chukulia hiyo kama fursa ya kujua ambacho kimekuwa ndani yako kwa muda mrefu, kisha anza mabadiliko kwenye fikra zinazotawala akili yako kwa muda mrefu.

Kwa njia hiyo utakuwa mtu bora ambaye hata upitie hali gani, bado utafanya yaliyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha