Wakati vifo vya ugonjwa wa Ukimwi vilipokuwa vinapamba moto, kipindi ambacho dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo zilikuwa hazipatikani kwa urahisi na kwa wote wenye maambukizi, mtu aliyepata maambukizi aliitwa anaishi kwa matumaini.

Ni kama vile mtu akishapata virusi hivyo basi ana tiketi ya uhakika ya kifo na hivyo siku zilizosalia ni za kuishi kwa matumaini. Huu ulikuwa unyanyapaa ambao kwa sasa umekosa nguvu, siyo kwa sababu Ukimwi umeisha, ila kwa sababu wagonjwa wanatumia dawa na siyo rahisi kuwajua kwa nje.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba kila mtu anaishi kwa matumaini, kwa sababu iwe una ugonjwa au la, hakuna mwenye uhakika na kesho.

Wote tunajua jinsi ambavyo kuna watu wanaweza kuwa hoi kitandani na watu wakawa wanasubiri siku ya kupewa taarifa kwamba amefariki, lakini hao wanaosubiri wanakuwa wa kwanza kufariki na kuwaacha walio hoi.

Lakini zaidi, mfumo mzima wa maisha, jamii, biashara na uchumi, umejengwa juu ya matumaini.

Tuanze na fedha, hebu fikiria nini kinaipa fedha thamani, nini kinafanya uite karatasi nyekundu elfu kumi na nyeupe elfu moja? Ni matumaini, kwamba wengine nao wanachukulia hivyo. Kama watu wote wataacha kuamini kwenye thamani ambayo wanaambiwa fedha inayo, inakosa thamani hiyo mara moja.

Twende kwenye biashara, zaidi ya asilimia 80 ya biashara zote mpya zinazoanzishwa zinakuwa zimekufa ndani ya miaka mitano ya kuanzishwa kwake. Hii haijaanza leo, imekuwepo tangu mfumo wa ubepari umekuwa unatumika. Lakini kila siku watu wanaingia kwenye biashara, ni kwa sababu ya matumaini.

Mfumo mzima wa uchumi na ubepari umejengwa kwenye matumaini, watu wakipoteza matumaini hayo, kila kitu kinaanguka. Wale wanaoingia kwenye biashara na kushindwa ndiyo wanaochochea biashara kuendelea, la sivyo biashara zingedumaa.

Unapoingia kwenye biashara kipindi cha mwanzo ni cha mateso, unafanya kila kitu peke yako huku ikiwa hakuna faida unayotengeneza. Kinachokufanya uendelee ni matumaini unayokuwa nayo kwenye biashara hiyo, yanayotokana na ndoto kubwa uliyonayo, ambayo unaiona kabisa mbele yako.

Pamoja na kwamba hakuna anayeijua wala kuwa na uhakika na kesho, matumaini tuliyonayo leo yanatusukuma kupiga hatua zaidi.

Mmoja amewahi kusema jifunze kama utaishi milele, fanya kama utakufa kesho, ni njia nyingine ya kutupa matumaini ya kuendelea.

Kila mtu anaishi kwa matumaini, je ni matumaini gani uliyonayo wewe? Maana ukishakosa matumaini, hapo ndipo habari yako imeishia, utakata tamaa na kukosa nguvu ya kuendelea na mapambano. Huwezi kufanikiwa kwenye maisha kama huna matumaini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha