Kila uovu huwa unaanza kwa nia njema, lakini kwa sababu ya udhaifu wetu binadamu, huwa hatujui wakati gani nia njema inakuwa na madhara, tunaendelea kufanya tunachoamini ni sahihi wakati siyo sahihi.
Ndiyo maana katiba na sheria zimewekwa, ili kuhakikisha hata kama mtu ana nia njema kiasi gani, udhaifu wake binafsi haupelekei kuleta madhara.
Ni pale mtu anapoamua kuachana na katiba na sheria kwa sababu anaona ni kikwazo kwake kutimiza nia yake njema, ndipo uovu unapoanza kujitengeneza. Na kwa sababu sheria hazifuatwi tena, hata pale makosa yanapofanyika, hakuna anayeweza kuyakemea au kukosoa, kwa sababu hakuna sheria inayotumika.
Sasa ni rahisi kuliona hili kisiasa, kwenye tawala za nchi na dunia, lakini ni vigumu kuliona kwako wewe binafsi. Na lengo la kukukumbusha hapa leo ni kuangalia kwako binafsi.
Unapaswa kuwa na misingi unayoendesha nayo maisha yako, misingi ambayo unaifuata mara zote.
Kisha unapaswa kuwa na nidhamu binafsi ya hali ya juu sana, nidhamu ya kukusukuma kufanya kile kilicho sahihi.
Baada ya hapo, jitese, siyo kwa kujiumiza, bali kwa kufuata misingi yako kwa nidhamu kubwa na kutokuivunja kwa namna yote ile.
Nasema ujitese kwa sababu kuna wakati utataka kufanya kitu cha kukupendeza, kwa nia njema kabisa, lakini kiko nje ya misingi yako. Kamwe usivunje misingi hiyo kwa sababu ya nia njema ya mara moja.
Ukishavunja mara moja, ni rahisi kuvunja tena na tena na utafika mahali kuvunja inakuwa sehemu ya maisha yako. Inapofika wakati uvunjaji wa misingi yako ni kitu cha kawaida, unakuwa kwenye hatari kubwa.
Nia njema haipaswi kuvunja misingi uliyojiwekea, maana misingi uliiweka kwa fikra timamu, ila kinachokusukuma kwa nia njema huwa ni hisia zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli kabisa tumekuwa tunakimbilia kufanya kilicho rahisi badala ya kufanya kilicho sahihi.
Makala nzuri sana hii Kocha. Ahsante!
LikeLike
Karibu Datius.
LikeLike