Kile unachotafuta sana kwenye maisha yako, kinapatikana pale penye watu wachache wanaokitafuta pia.
Na sehemu pekee yenye watu wachache, ni ile ambayo siyo rahisi, ambayo inahitaji kazi na uvumilivu kupata unachotaka.
Kama tunavyojua, watu wanapenda urahisi na njia ya mkato kupata wanachotaka, hivyo hawapo tayari kuweka kazi na kujipa muda.
Wanakimbilia popote wanaposikia ni rahisi na kwa haraka na kuacha kule ambapo ni kugumu na kunakohitaji muda.
Wanajikuta wote wamekusanyika eneo moja na hivyo chochote kinachopatikana wanagawana na hakuna anayenufaika kwa kiwango kikubwa.
Sasa wewe ukiacha kwenda kwenye mkusanyiko wa wengi na kwenda kule ambapo wengi hawapakimbilii kwa sababu siyo rahisi na haraka, unaondokana na ushindani mkubwa na unapopata, unapata kwa kiwango kikubwa kwa kuwa hakuna wengi wanaoshindana na wewe.
Iwe ni kwenye kazi au biashara, kuna maeneo wengi wanayakimbia kwa sababu ya ugumu na uchelewaji wake na kuna maeneo wengi wanayakimbilia kwa sababu ya urahisi na uharaka wake. Wewe nenda kinyume na wanapokimbilia wengi na utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.
Lakini pia lazima kiwe kitu sahihi, usitake tu kutofautiana na wengine kwa sababu unataka kutofautiana, bali tofautiana nao pale penye manufaa makubwa lakini siyo rahisi.
Kwa sababu kila mtu anatembea kwa miguu, haimaanishi wewe utembee kwa mikono ili uwe tofauti. Bali unaweza kutembea kwa miguu kama wengine, lakini ukatembea kwa namna ya tofauti na wengine.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako, kwa kuangalia maeneo yenye fursa nzuri ya wewe kufanikiwa na ambayo hayana msongamano wa watu, kisha kuweka kile unachopaswa kuweka ili kupata unachotaka kupata.
Hili siyo rahisi, ndiyo maana wachache pekee wanafanya na wachache hao ndiyo wanaopata mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kweli umeelezea vyema dhana hii ya kujitofautisha na wengine.
Ubarikiwe sana Kocha.
LikeLike
Karibu Datius.
LikeLike
Maandalizi ni eneo moja ambalo hakuna watu wengi. Maandalizi yanahitaji subira na uvumilivu ambavyo ni wachache wenye sifa hizi ambazo ni muhimu kupata mafanikio. Ukiziishi hizi lazima utakuwa wa tofati.
LikeLike
Asante sana Mbise,
Hiyo ni kweli, watu hawana kabisa muda wa kujiandaa, hivyo ukiwa na maandalizi mazuri, utaweza kuitumia vizuri kila fursa kuliko wengine.
LikeLike
Asante kocha , kuwekeza ndani yangu kwa maarifa sahihi na kuyafanyia kazi na kujipa muda ni vitu tufauti lakini sio vinavyofanywa na wengi
LikeLike
Hakika.
LikeLike