Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa.

Leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi mtu unavyoweza kutumia kipaji chako kuwa ajira inayokuingizia kipato kizuri cha kukuwezesha kuyaendesha maisha yako.

Kuna kauli inasema kwamba kuna uhaba wa ajira, lakini hakuna uhaba wa kazi. Kinachowasumbua wengi ni kufikiria tu ajira rasmi za kupewa na wengine, badala ya kuangalia ni kazi gani wanazoweza kufanya.

Watu wana changamoto na mahitaji mbalimbali, ukiangalia hivyo na kujua unachoweza kufanya kuwatatulia changamoto zao au kutimiza mahitaji yao hutakosa kitu cha kufanya.

Na sehemu nzuri ya kuanzia ni kwenye kipaji ulichonacho, kila mmoja wetu kuna kitu ambacho anaweza kukifanya vizuri kuliko wengine na yuko tayari kukifanya hata kama hakuna anayemlipa.

Hicho ndiyo kipaji cha mtu, na kabla hatujaingia kwenye ushauri wa jinsi ya kukitumia, hakikisha unatafakari hapa kipaji chako ni kipi kama bado hujakijua.

Kabla ya kuingia kwenye ushauri wa leo, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Dr pole na shughuli za kila siku, binafsi na kushukuru sana kwa elimu ninayoipata kwako.

Mimi ni mpambanaji ambaye nimehitimu ualimu, baada ya kutokea suala uchelewaji (ukosekanaji) wa ajira za moja kwa moja mwaka mmoja baada ya kuhitimu, nikaamua kuomba mtaji kwa mzazi na nikafungua saluni ya kunyoa nywele.

Kipaji changu ni Sanaa ya kuongea (folklope) & muziki .

Lakini jambo ambalo limekuwa gumu kwangu na tofauti na matarajio yangu ni kwamba nimeshindwa kunyanyua muziki wangu na kufungua biashara nyingine kama nilivyokuwa nikiwaza awali. Lakini nimekuwa nikiweka juhudi kila siku katika muziki nikiamini nitapata mafanikio makubwa katika muziki.

Changamoto kubwa ni kwamba kipato ninachoingiza kwa sasa kinatosheleza mahitaji ya kila siku na kuishia kuendesha familia na biashara yenyewe na inakuwa ngumu kupiga hatua kubwa.

Nimewahi kurekodi nyimbo 4 lakini nyimbo hizo hazijulikani kwa sababu sijazi promote. Naamini nikipromote kazi zangu nikafanya na nyingine nyingi nitapata fursa ya kuuaga umaskini, nitaajiri vijana katika saluni na kufungua saluni nyingi kuajiri wengi ili nikuze mtandao wangu. – Elick J. K.

Nianze kwa kukupongeza rafiki yetu Elick kwa kuamua kuchukua hatua, kuamua kutokusubiri mpaka upate ajira badala yake ukaanza kujishughulisha.

Nakupongeza kwa sababu mwingine angesemana ualimu wangu siwezi kwenda kuwa kinyozi mimi, hiyo siyo kadhi ya hadhi yangu kwa elimu niliyonayo.

Kama ambavyo nimekuwa ninasema, kama huna kazi na huna fedha, huna hadhi, hivyo acha kujidanganya na tafuta mahali pa kuanzia.

Kwa mwenzetu ameshapata pa kuanzia na hivyo ni vizuri.

Kwa wale ambao wana kipaji na hawana kazi yoyote wanayofanya, tafuta mahali pa kuanzia, fanya kazi yoyote halali itakayokuingizia kipato, hata kama ni kuwa kibarua kwenye shughuli za kutumia nguvu kama ujenzi au kilimo.

Ni lazima uwe na kitu kingine unachofanya cha kukuingizia kipato kwa sababu kipaji chako kinahitaji muda mpaka kiweze kukuingizia kipato.

Kabla sijaendelea nisisitize kwamba kipaji siyo njia ya mkato ya kufikia utajiri na mafanikio makubwa.

Baada ya kuwa na shughuli unayofanya ya kukuingizia kipato, yashushe sana maisha yako, punguza mambo mengi mno. Fanya yale ya msingi tu na mengine achana nayo. Uko kwenye kipindi cha vita hivyo lazima uendeshe maisha yako kimkakati.

Hili lina faida mbili, ya kwanza ni kufanya matumizi yako kuwa madogo kuliko kipato na hivyo utaweza kujidundulizia akiba ya kupiga hatua zaidi. Faida ya pili ni kupata muda wa kufanyia kazi kipaji chako.

Kumbuka hapo unaendelea na shughuli zako za kukuingizia kipato huku pia ukifanyia kazi kipaji chako. Kwenye kitabu cha BIAHARA NDANI YA AJIRA ni dhana ninayoiita KUWA NA SIKU MBILI NDANI YA SIKU MOJA. Siku ya kwanza ni ya shughuli yako inayokuingizia kipato na siku ya pili ni ya kufanyia kazi kipaji chako.

Kwa mwenzetu Elick tayari ameshaanza kufanyia kazi kipaji chake, kwani amesharekodi nyimbo nne, yuko pazuri kabia.

Kwa mwingine fanyia kazi kipaji chako, kama ni mwandishi anza kuandika, fungua blog na andika kila siku au anza kuandika kitabu chako. Kama ni mnenaji jifunze unenani na tafuta fursa za kunena. Kama ni mshauri jifunze eneo unalotaka kuwashauri wengine na angalia wenye uhitaji na uwape ushauri.

Kwa kipaji chochote ulichonacho, fanya mambo mawili kila siku, jifunze zaidi kuhusu kipaji hicho kupitia usomaji wa vitabu na anza kufanyia kazi kwa kuangalia watu wana uhitaji gani kisha kuwapa kulingana na kipaji chako.

Hapa panahitaji kazi na muda, siyo kitu cha haraka na hakuna atakayekuwa tayari kukulipa mwanzoni, kwa sababu wengi hawajui una nini hasa. Ni mpaka waone matokeo unayozalisha ndiyo wawe tayari kukulipa. Hivyo utahitaji kuzalisha matokeo makubwa bure kabisa kabla hujawaambia watu wakulipe.

Una shughuli inayokupa kipato cha kuendesha maisha, umeyarahisisha maisha na umeanza kufanyia kazi kipaji chako. Hizo ni hatua muhimu kabisa, lakini kuna adui anakuwa kikwazo kwako ambaye usipomvuka kipaji chako hakiwezi kukunufaisha.

Adui huyo ni kutokujulikana. Wewe una kitu ambacho kina manufaa kwa wengine, lakini wale wanaokihitaji sana hawajui kuhusu uwepo wako. Na hapo ndipo unapohitaji kutangaza kazi yako ili iwafikie wengi.

Hapa ndipo mwenzetu Elick alipokwama, nyimbo tayari anazo lakini hajazitangaza. Na kuna wengi kama yeye, wana vipaji, wana kazi nzuri lakini hawazitangazi.

Hii inaweza kutokana na fikra ambazo mtu anakuwa nazo kwenye kutangaza kazi, wengi husubiri waweze kutangaza kwenye vyombo vikubwa vya habari ili kuwafikia wengi kwa pamoja. Hilo linakuwa linashindikana kwa sababu ya mtaji.

Lakini tushukuru zama tunazoishi ni zama za maarifa na taarifa ambapo mtandao wa intaneti umerahisisha sana mawasiliano baina ya watu na usambaaji wa taarifa.

Hivyo kutangaza kazi yako siyo kikwazo tena, ila unachohitaji ni mkakati. Wengi wamekuwa wanasambaza kazi zao kwenye mitandao ya kijamii wakitaka kila mtu aone, na matokeo hayawi mazuri kwani watu wamevurugwa kwenye mitandao hiyo na hawana muda kabisa.

Mkakati mzuri wa kufanyia kazi kwenye kutangaza kazi zako ni kuanza na watu ambao unawalenga, watu ambao wana uhitaji kweli au wanapendelea kitu hicho, kisha kuwakaribisha wafuatilie kazi zako. Anza na watu wachache wanaoelewa kweli kazi unayoifanya.

Kwa muziki wa rafiki yetu Elick, anza na watu ambao watauelewa, wataufurahia na kuburudika nao. Hao wachache wakipendezwa watakuwa tayari kuwakaribisha wengine. Njia ya watu kukaribishana ina nguvu kuliko wewe kutumia nguvu kubwa kutaka kumfikia kila mtu.

Lakini njia hii ni ndefu na inahitaji muda, ndiyo maana nimekutahadharisha mapema kwamba itakuchukua muda mpaka uweze kuingiza kipato kwa kipaji chako.

Anza na watu wachache, wanaoielewa kweli kazi yako na wanaonufaika nayo. Na hao waombe wawaalike wengine nao kuja kunufaika. Jenga nao mahusiano mazuri kiasi cha kuwa mnasafiri pamoja, hilo litakusaidia kuwa na wafuasi au hadhira inayokuamini na kukusikiliza.

Hiyo ni kwa kila aina ya kipaji ulichonacho, iwe uandishi, ushauri, unenaji na hata bishara nyingine yoyote unayokuwa unapendelea kufanya, anza na wateja wachache, wahudumie vizuri mno kisha waombe wakuletee wateja zaidi. Wateja wanaoletwa na wateja walioridhika, huwa ni wateja bora kabisa.

Kutangaza kazi moja haikutoshi kuwa na uhalali wa kuingiza kipato kwa kipaji chako, badala yake unahitaji kuendelea kutoa kazi nyingine ambazo ni bora zaidi. Kwa kuwa umeshaanza na watu fulani, unazidi kuwajua nini wanataka au wapi wanakwama, hivyo waandalie kazi inayowasaidia kuweza kupiga hatua zaidi.

Kila kazi mpya unayoitoa inatangaza zaidi kazi zako, inaleta watu wapya zaidi kwako na unaendelea kukuza jumuia uliyoitengeneza kwenye kazi zako.

Baada ya kuwa na jumuia kubwa au wafuasi wengi ambao wanafuatilia kazi zako, sasa unaweza kuanza kuingiza kipato. Anza kwa kutoa kazi ambazo ni bora zaidi na ambazo wafuasi wako watakuwa tayari kukupa fedha.

Katika kulipwa una njia tatu za kuchagua; moja ni kuwaomba wafuasi wako wakuchangie ili huduma iendelee. Mbili ni kutoa kazi ambazo utaziuza kwa wafuasi wako. Na tatu ni kuendelea kuwapa wafuasi wako vitu vya bure, lakini kuwapa wengine nafasi ya kuwatangazia wafuasi wako biashara zao.

Njia zote tatu zinafanya kazi, ila nashauri utumie ya kwanza na ya pili, hakuna ubaya kwenye kutumia ya tatu, ila kama unawaheshimu wafuasi wako, usiwauze kwa wengine, wape kazi bora na wakuchangie au wauzie kazi ambazo ni bora kabisa.

Unaweza pia kuwa na bidhaa nyingine zinazoendana na kipaji chako na wafuasi wako wakanunua kukuunga mkono. Mfano kwenye muziki badala tu ya kuwa na muziki, unaweza kuwa na mavazi yenye chapa yako, ambayo utawashawishi wafuasi wako kununua ili kujitambulisha kama jamii inayofuatilia kazi zako.

Ukishakuwa na ubunifu wa kuweza kutumia kipaji chako kupata wafuasi na kujenga jamii, ubunifu huo huo utakuonesha njia mbalimbali za kuingiza kipato. Muhimu ni uhakikishe kuingiza kwako kipato hakuharibu jumuia uliyoitengeneza kwa kipaji chako. Maana huo ndiyo mtaji wako ambao unapaswa kuendelea nao ili kufanikiwa zaidi.

Mwisho kabisa nikutake uendelee kujifunza, kwa shughuli ya kukuingizia kipato unayofanya, ifanye vizuri ili kuingiza kipato cha kutosha. Pia wewe mwenyewe kazana kuwa bora zaidi kila siku. Na tangu awali, kazana kujijengea uhuru wa kifedha ili uwe huru kufanyia kazi kipaji chako.

Kuna vitabu vitatu muhimu sana unavyopaswa kuvisoma kwenye hili;

Cha kwanza ni UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, hiki kitakuwezesha kujua nguvu kubwa iliyo ndani yako na jinsi ya kuitoa kwenye kipaji chako.

Cha pili ni BIASHARA NDANI YA AJIRA, hiki kitakusaidia kuweza kufanya yote mawili kwa pamoja na kinakusaidia kwenye kudhibiti vizuri muda wako na hata kujua wakati sahihi wa kuachana na shughuli nyingine unayofanya na kuweka nguvu zako zote kwenye kipaji chako.

Kitabu cha tatu ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, hiki kitakusaidia kuanza kujijengea uhuru wa kifedha mapema kabisa ili uzidi kuwa huru kufanyia kazi kipaji chako.

Kupata vitabu hivyo vitatu wasiliana na 0752 977 170 sasa hivi.

Rafiki yangu mpendwa, nikuambie tu kwamba inawezekana kabisa kugeuza kipaji chako kuwa kazi inayokuingizia kipato. Unachohitaji ni mkakati sahihi, kuweka kazi na kujipa muda. Makala hii imekupa mwanga mkubwa, tengeneza mkakati wako na anza kuweka kazi, badaye utajishukuru kwa hatua ulizoamua kuchukua. Usiache kusoma vitabu vitatu nilivyokushirikisha hapo juu.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp