Serikali ya India ilikuwa na tatizo la nyoka, nyoka walikuwa wengi kiasi cha kuhatarisha usalama wa watu. Njia mbalimbali za kuwatokomeza hazikufanikiwa. Mwisho wakajaribu njia ya kuwashirikisha wananchi, ambapo mtu aliyepeleka nyoka aliyekufa, alilipwa fedha.

Njia hiyo ilifanya kazi, kwani kwa kipindi kifupi nyoka walipungua sana. Lakini cha kushangaza, nyoka hawakuisha kama ilivyotegemewa. Kwani kila siku watu walikuja na nyoka zaidi ili walipwe.

Serikali iliamua kufanya uchunguzi kwenye hilo na kugundua kuna watu walikuwa wanazalisha nyoka na kuwauza. Hivyo watu walienda kununua nyoka hao na kuwaua kisha kupeleka serikalini kupata fedha.

Watu wana tabia ya kutafuta njia ya mkato ya kujinufaisha zaidi, hivyo kunapokuwa na motisha yoyote, jua kabisa watu watapata njia ya kujinufaisha nayo zaidi.

Hivyo kuwa makini sana na motisha unaotoa kwa watu, hakikisha kuna njia ya uhakika ya kupima kwa usahihi kile unachotaka kitokee. Pia ondoa kabisa mianya yote ya watu kufikia njia ya mkato ya kujinufaisha zaidi.

Matapeli pia wamekuwa wanatumia mwanya wa motisha kujinufaisha zaidi, huwa wanajua watu wanapenda kutafuta njia za mkato za kujinufaisha, hivyo wanatumia hilo kujinufaisha. Ipo mifano mingi na ambayo imekuwa inatumia njia za tofauti tofauti, lakini njia kubwa ni ile ya mtu kwenda kwenye kijiji na kutangaza kununua mazao kwa bei juu. Wauzaji wa mwanzo anawalipa vizuri, ila baadaye watu wanapokuja kuuza wengi anawataka walete mzigo kisha watalipwa baadaye. Kwa kuwa kila mtu anataka kumuuzia mazao yake, uhaba unatokea, basi mtu huyo anakuwa na watu ambao wanachukua mazao yaliyoletwa na watu na kwenda kuwauzia tena. Baada ya muda matapeli hao wanaondoka, wakiwaacha watu na maumivu mara mbili, mazao na fedha zao pia.

Kujua hili, kunakukinga na mengi, jua penye kila motisha wa kupata fedha, watu watatumia njia za mkato kujinufaisha zaidi, ni wajibu wako kuhakikisha hilo halikuumizi wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha