Biashara zote zinazoshindwa, huwa zinakuwa zimepitia moja au baadhi ya sababu hizi tano.
Moja ni kutokujulikana, wateja hawajui kama biashara ipo na hivyo hawaji kununua. Hapa tatizo ni masoko hayafanyiki kwa uhakika, hivyo biashara inakuwa na bidhaa au huduma nzuri, lakini wanaolengwa hawajui kama ipo. Dawa ya hii ni kuwa na mkakati wa masoko ambao ni endelevu, ili biashara iwe inawafikia wateja wapya kila wakati.
Mbili ni udogo, kama biashara ni ndogo sana, inashindwa kutengeneza faida ya kutosha kuweza kujiendesha yenyewe. Dawa hapa ni kuhakikisha biashara inaendelea kukua hata kama imeanzia chini.
Tatu ni kasi ya ukuaji kuwa ndogo, biashara inaweza kuwa inakua, lakini kasi yake isiridhishe, hasa ukizingatia na mambo mengine ya nje, kama ushindani na mabadiliko ya teknolojia. Dawa hapa ni kuhakikisha biashara inakua kwa kasi kubwa ili iweze kuendana na ushindani na mabadiliko ya teknolojia.
Nne ni uwekezaji usioridhisha, kama hakuna uwekezaji endelevu unaoendelea kufanyika kwenye biashara, inakufa. Dawa hapa ni uwekezaji kuendelea, kila sehemu ya faida inapaswa kurudi kwenye biashara kama uwekezaji. Pia kutafuta vyanzo vingine mbadala ili kuwekeza zaidi kwenye biashara.
Tano ni gharama za uendeshaji kuwa kubwa kiasi cha faida halisi kutokupatikana. Gharama zisipodhibitiwa na kubajetiwa vizuri, huwa zinaendelea kukua kadiri biashara inavyokua. Dawa hapa ni kujua yale muhimu na kuyawekea bajeti ili gharama zisikue sana kadiri biashara inavyokuwa.
Kwa kujua haya matano yanayoua biashara nyingi, utaweza kuilinda biashara yako isife.
Na kama biashara yako inanyemelewa na yoyote kati ya hayo, ni wakati wa kuchukua hatua sahihi sasa ili isifikie kifo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Upo sahihi sana kocha
Ukifanya biashara upo darasani muda wote unatakiwa kitafakari mwenendo wa biashara yako.
#binti lips
LikeLike
Karibu Mary.
LikeLike