James Altucher, mwandishi na mwekezaji wa nchini Marekani amekuwa akiandika kuhusu makosa mbalimbali aliyofanya kwenye maisha yake na yakapelekea apate matokeo mabovu pamoja na kuingia kwenye matatizo makubwa.
Amekuwa akieleza kwamba ameshaanzisha biashara 20, 18 kati ya hizo zikashindwa kabisa.
Anaeleza amewahi kuuza kampuni yake na kuwa milionea, lakini miaka michache baadaye akawa amepoteza fedha zote na kufilisika kabisa.
Amewahi kuwa na nyumba yake anayoimiliki, lakini akaipoteza na kujikuta akilala mitaani kwa kukosa makazi.
Amekuwa anaeleza jinsi ndoa zake mbili zilivyoishia kwenye talaka.
Na mengine mengi, lakini katika yote haya, huwa hamlaumu mtu mwingine yeyote isipokuwa yeye mwenyewe. Anakiri wazi kwamba ujinga na uzembe wake ndiyo umekuwa unamuingiza kwenye matatizo mengi anayoyapitia.
Na japokuwa matatizo hayo yamekuwa yakimtikisa hasa, ameweza kujenga mhimili ambao huwa hautikiswi na chochote. Mhimili huo ndiyo umekuwa unamsaidia kuweza kuinuka tena hata anapokuwa ameanguka.
Mhimili wake huwa anauita DAILY PRACTICE, yaani vitu anavyovifanya kila siku kwenye siku yake bila ya kujali nini kinaendelea kwenye maisha yake.
Na msingi mkuu wa zoezi hilo ni kujiboresha kwa asilimia moja kwenye maeneo haya manne;
Eneo la kwanza ni afya ya mwili, hapa anaweka mkazo kwenye kula kwa usahihi, kufanya mazoezi na kupata muda wa kutosha kupumzika.
Eneo la pili ni afya ya hisia, hapa anaweka mkazo kwenye kuzungukwa na watu anaowapenda na wanaompenda.
Eneo la tatu ni afya ya ubunifu, hapa anaweka mkazo kwenye kufanya kitu cha kibunifu kila siku na kuandika mawazo 10 juu ya chochote kila siku.
Eneo la nne ni afya ya kiroho, hapa anajisalimisha kwenye nguvu kubwa kuliko yeye na kutengeneza utulivu wa ndani unaomwezesha kukabiliana na chochote.
Hivyo ndivyo James ameweza kutengeneza mhimili usiotikiswa na umemwezesha kusimama kila anapoanguka.
Je wewe ni mhimili gani unajijengea kwenye maisha yako?
Kwa sababu lazima utaanguka, hata kama umejipanga na kujiandaa kiasi gani, hata kama utafanya kila kilicho sahihi, bado utaanguka. Kama huna mhimili imara ndani yako, ukishaanguka ndiyo habari yako itakuwa imekwisha.
Jijengee mhimili imara kwa kuwa na vitu unavyovifanya kila siku bila ya kujali unapitia nini. Inaweza kuwa kitu chochote, lakini lazima ukifanye kwa kusudi, lazima ukifanye kama sehemu ya matumaini kwamba maisha yako hayajaisha na usiache kufanya hata siku moja.
Kama umekuwa unafuatilia mafunzo haya ninayotoa, tayari unajitambua, unajijua ni nani, unataka nini na kusudi lako ni lipi. Sasa jenga mhimili imara kwako ambao hautatikiswa na chochote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha
Leo umenipa kitu kikubwa sana
Naanza kukimbia tena kumbe hata kama nafanya kilicho sahihi bado nitapitia hali ya kuanguka
#binti lips
LikeLike
Karibu Mary
LikeLike