Zama tunazoishi sasa ni zama za mvurugano, ni vigumu mno kupata utulivu wa kufanya jambo lolote lile unalopanga kufanya.

Tunazungukwa na usumbufu mwingi ambao unaingilia mengi tunayopanga kufanya, kitu kinachoathiri ufanisi na uzalishaji wetu.

Unaweza kuhangaika kupangilia mambo yako mengi, lakini kwa usumbufu unakuzunguka usiweze kuyafanya mambo hayo.

Wengi wamekuwa wanafanya mambo mengi bila kuyakamilisha, wanagusa hili wanaacha, wanagusa lile wanaacha. Mwisho wa siku wanakuwa wamechoka na hakuna walichozalisha.

Njia pekee ya kukabiliana na hili la usumbufu huku ukiongeza ufanisi na uzalishaji wako ni kuchagua kuweka umakini wako wote kwenye kitu kimoja ulichochagua kufanya.

Katika mengi unayotaka kufanya, yapange kwa vipaumbele, chagua kile ambacho ni muhimu kuliko vyote, kisha weka umakini wako wote kwenye kufanya kitu hicho kimoja.

Wakati unakifanya, ondoa kabisa kila aina ya usumbufu, kama ni simu izime au iweke kwenye utulivu, kama ni watu basi nenda eneo ambalo hakuna watu au waliopo hawakujui.

Tumia kila njia uweze kupata muda ambao umakini wako wote utakuwa kwenye kitu kimoja ulichochagua kufanya. Ukiweza kufanikisha hili, utafanya makubwa kwa muda mchache kuliko unayoweza kufanya ikiwa muda wako umegawanyika kwenye usumbufu mbalimbali.

Weka kila kitu kwenye jambo moja ulilochagua kufanya kwa muda uliochagua kulifanya, ukishamaliza ndiyo uende kwenye jambo jingine na kurudia kufanya kwa umakini kama huo.

Mambo ya kufanya ni mengi, muda ulionao una ukomo, huwezi kufanya kila kitu, ila unaweza kufanya yale machache na muhimu, weka kipaumbele na umakini kwenye hayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha